CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakitishwi na propaganda zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kushirikiana na mamluki wake, zenye lengo la kukichafua na kujenga uhalali wa kuzuiliwa kwa maandamano na mikutano ya chama hicho.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa masuala ya Bunge na Halmashauri wa CHADEMA, John Mrema, alisema vyama vidogo vya Cuf, NCCR-Mageuzi, TLP na UDP vimo katika utekelezaji wa mkakati huo wa CCM, kwa kushirikiana na kikundi maalumu kilichoundwa kwa ajili hiyo, kinachopachikwa jina la ‘vijana wapenda amani.’
Alisema, mwanzoni mwa mwaka huu walitoa taarifa kwa umma wakieleza kuwa Chama cha Wananchi (CUF) si chama cha upinzani, kwa kuwa kinashirikiana na CCM na sasa ushahidi unazidi kujionyesha waziwazi, kwa mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, kutoa matamko ya kuunga mkono propaganda za CCM zinazoituhumu CHADEMA kuwa inahatarisha amani ya nchi.
“CUF wamefunga ndoa na CCM, hivyo si chama cha upinzani …ni CCM B, kwa hiyo hatushangai kuona chama hicho na mwenyekiti wake wakiishambulia CHADEMA…wanatekeleza mkakati wao wa pamoja.
“CHADEMA ni chama makini kinasimamia na kutekeleza majukumu yake kwa umakini, hivyo hivi vyama vingine vinavyojiita vya upinzani tulishavitilia shaka muda mrefu hata wakati wa kuunda kambi ya upinzani tulibaini hawana dhamira ya kweli,” alisema.
Alisema kwa sasa CCM imepoteza mwelekeo na imedhohofika ndiyo maana inafikia hatua ya kutumia watu mbalimbali ili waisaidie kuishambulia CHADEMA inayoungwa mkono na wananchi wengi.
Alisema haiingii akilini kuona vijana wanaotaabika na hali mbaya ya maisha wakinunuliwa kufanya maandamano na mikutano yao inayolenga kuwatetea, na kwamba wana taarifa kuwa kikundi hicho kimenunuliwa na kina uhusiano wa karibu na vigogo.
“Hivi kweli linajitokeza kundi la vijana na kudai wanaandaa maandamano ya kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete aliyoitoa Februari wakati leo tupo mwezi Machi? Wananchi wajiulize kwanini …sisi tunajua yote yanayoendelea,” alisema Mrema.
Alisisitiza kuwa CHADEMA hawababaiki na hatua hiyo bali kwa sasa wanajipanga zaidi katika kuhakikisha wanasema ukweli kwa kufanya maandamano na mikutano katika maeneo mengine ya nchi.
Alisema chama hicho kipo katika hatua za mwisho kuhakikisha wanamalizia vikao vilivyobaki, ikiwa ni pamoja na kutoa ratiba ya wapi wanaelekea baada ya kumaliza maandamano yao katika maeneo ya Kanda ya Ziwa.
No comments:
Post a Comment