POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam wamemkamata Katibu Muhtasi wa Ubalozi wa Canada, Jean Touchatte (48) kwa tuhuma za kuwatemea mate askari wa Usalama barabarani na Mwandishi wa Habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) .
Touchatte anatuhumiwa kumshambulia askari wa usalama barabarani aliyekuwa akiongoza magari katika eneo la Banana wilaya ya Ilala.
Kaimu kamanda wa kanda hiyo, Charles Kenyela, amesema, mtumishi huyo wa ubalozi anadaiwa kufanya makosa hayo Desemba 9 saa 8.45 mchana wakati askari huyo namba E 1653, Koplo Samson akiwa kazini maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Kenyela, wakati akiendelea kuyaruhusu magari yanayotokea Ukonga kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Touchatte alifika eneo hilo akiwa anaendesha gari lenye namba za usajili T 17 CD 178 Toyota Land Cruiser Prado mali ya Ubalozi wa Canada.
Amesema, mtuhumiwa huyo alikuwa anatoka Ukonga kwenda uwanja wa ndege, ghafla alipunguza mwendo, akafungua kioo cha gari lake na kumtemea mate askari huyo.
Kenyela amedai kuwa,kitendo hicho kiliwashangaza wengi walioshuhudia,na kwamba sababu ya kufanya hivyo haikufahamika, hivyo polisi wa doria walipewa taarifa ili kulifuatilia gari hilo.
“Askari wetu walianza kufuatilia kwa nyuma gari hilo na walipofika barabara ya Nyerere karibu na Kamata gari hilo lilikamatwa na kupelekwa moja kwa moja hadi makao makuu ya polisi Trafic Kanda Maalum ya Dar es Salaam na kuwekwa chini ya ulinzi” amesema.
Kwa mujibu wa Kenyela, wakati mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa,waandishi wa habari akiwemo Jerry Muro(29) wa TBC walifika kituoni hapo, wakitaka kufahamu nini kilichotokea ndipo mtuhumiwa huyo akamtemea mate sehemu ya chini ya kidevu chake na kusambaa katika flana aliyokuwa amevaa.
Muro alifungua jalada la shambulio CD/IR/4818/2009, na kwa mujibu wa Kenyela, mtuhumiw alipohojiwa hakuwa tayari kujibu wala kutoa maelezo yake kwa madai kwamba mpaka balozi wake awepo.
No comments:
Post a Comment