Monday, November 9, 2009

Mwanamke 'mzuri'

KUNA mdau kanitumia huu ujumbe, alichokisema ni kweli?
KUNA wanaume wengi mitaani ambao leo hii licha ya kuwa na wake 'wazuri' wanalia kila kukicha.

Maisha yao ni ya kuumizwa kila siku, hawana furaha kabisa kutokana na tabia mbaya za wake zao.

Wanaume hao walidhani kuoa mwanamke mzuri ni furaha kumbe ni maumivu kwao. Waswahili walisema,si kila king’aacho ni dhahabu.

Kuna wanawake huko mtaani ukiwaona walivyoumbika utadhani malaika lakini tabia zao zinatia kinyaa.

Ni wanawake wasiotulia na mwanaume mmoja.

Na hata wale wanaobahatika kuolewa, hawatulii bado wanakuwa na tamaa za kijinga na waume zao wanapobaini kutotulia kwao huleta kiburi.

Kama huamini katika hili chunguza utabaini kwamba, baadhi ya wanawake walioolewa ambao ni wazuri na wanajijua wanawadatisha wanaume, hawaoni hatari kuachika.

Hii ni kwa sababu wanajua hata wakiachwa leo kesho atatokea mwanaume mwingine na kumtaka.

Si wana mvuto? Ndio maana baadhi yao wanakuwa viburi kwa waume zao.

Unapompenda mwanamke mzuri na ukatamani awe mkeo kwanza chunguza historia yake.

Je ni msafi kwa maana halisi ya usafi kitabia?
Familia yake ikoje? Kwa sababu isije ikawa mwanamke huyo
mzuri ni sawa na mchicha wenye mzuri lakini kumbe umeota kwenye kinyesi.

Wapo baadhi ya wanawake ukikutana nao barabarani utachanganyikiwa kwa uzuri wao lakini ukifuatilia unaweza kukuta familia anayotokea haina maadili mazuri.

Yawezekana ni walevi, wazinzi na wenye tabia zisizokubalika katika jamii.

Katika kutaka kuchukua hatua za kuanzisha uhusiano wa kutaka kuoa kabisa ni vyema ukawashirikisha watu wanaomfahamu vizuri huyo mwanamke.
Hao watakupa mwanga unaoweza kukusaidia aidha kuendeleza uhusiano wako ama kuusitisha.
Kamwe usidanganyike na uzuri wake kwa sababu uzuri si tija.

Chunguza kama naye anakupenda Hili liko wazi kwamba, unaweza kutokea kumpenda demu mkali sana na
ukamshawishi awe na wewe lakini kumbe yeye hana penzi la dhati kwako.

Ukilazimisha kwa pesa ama vishawishi vingine kwa mtu kama huyu, utakuwa unaingia kwenye penzi la kifo.

Fanya uchunguzi ili kubaini kama ana penzi la dhati na ukigundua hakupendi wala usilazimishe, muache labda kama unataka kustarehe naye tu kisha kumuacha lakini si wa kuoa.

Katika hili la kubaini kama mwanamke huyo analo penzi la dhati ni lazima mwanaume mwenyewe akajifahamu na kufahamu vigezo vya mpenzi anayemhitaji katika maisha yake.
Ifahamike kuwa kila mwanaume ana wake wa maisha. Hivyo asiyekufaa wewe anawafaa wengine, kinachotakiwa ni kujitambua kwanza ili umtambue umtakaye.

Wanaume wengi hawafahamu wanahitaji wapenzi wa aina gani, hivyo wanajikuta kama watu wanaoingia sokoni bila kujua wanataka kununua nini?
Ndiyo maana wengi wameangukia kwa matapeli wa mapenzi na mwishowe kuumizwa moyo yao bure.

Lingine analotakiwa kulifanya mwanaume ni kukaa chini kisha kuorodhesha vigezo stahili vya mwanamke unayemtaka.

Baada ya hapo orodhesha tena kasoro zake unazoweza kuzivumilia na zile ambazo huwezi kuzivumilia kabisa.
Hii inatokana na ukweli kwamba mwanadamu hajakamilika, kila mtu ana upungufu wake.

Katika kumalizia mada hii niseme tu kwamba, kwa wanaume wanataka kuoa si vibaya wakafahamu wanahitaji wanawake wa aina gani.

Je chagua lako ni mwanamke mzuri hata asiye na tabia nzuri? Je ni mwanamke mwenye tabia nzuri hata asiwe mzuri au mwaname mzuri na tabia nzuri pia?

Naamini kila mwanaume anataka mwanamke mzuri na mwenye tabia nzuri hivyo basi ili kujihakikishia maisha yenye furaha, unapomuona mwanamke mzuri, jiridhishe na upande mwingine wa tabia kisha utangaze sera za ndoa,
la sivyo utaishia kusifiwa una mke mzuri lakini ndani hapakaliki
.
Pamoja na yote aliyoyasema mdau, nina swali, mwanamke MZURI ni yupi? Unatumia vigezo vipi kusema mwanamke huyu ni mzuri au la?

1 comment:

  1. hata wanawake pia tunatafuta wanaume wenye tabia njema, sio wanaume peke yao wenye haki ya kuchagua hata wanawake nao lazima waangalie quality ya mwanaume nasio kubebwa tu.

    ReplyDelete