MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Frederick Werema(55),amesema ana msimamo na haogopi shinikizo la yeyote.
Werema amesema,Rais Jakaya Kikwete anafahamu kuwa ana msimamo na waliowahi kufanya kazi na yeye wanatambua kuwa hafanyi uamuzi kwa kushinikizwa.
“Bila shinikizo hakuna kazi,mimi ni mtu wa msimamo,aliyeniteua anajua msimamo wangu na hata waliowahi kufanya kazi nami wananijua sishinikizwi na mtu” amesema Werema muda mfupi baada ya Rais Kikwete kumuapisha Ikulu, Dar es Salaam.
Werema anafahamu kuwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu inahusishwa na rushwa katika kuingia mikataba ya Serikali lakini yeye amesema “ninaporidhika ndipo mikataba itatekelezwa sitaki kushinikizwa”.
Amesema,hana taarifa rasmi kwamba,ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inahusika kuingia katika mikataba mibovu.
“Mimi sifahamu taarifa hizo nasoma kwenye magazeti hivyo nahitaji kufanya utafiti wa kutosha na kuwasiliana na taasisi nyingine za Serikali kupata taarifa kamili ndipo nijue kama nachukua hatua”.amesema.
Werema ana taaluma ya sheria ya biashara,namna ya kujadiliana katika mikataba na namna ya kufanya biashara ya umeme katika kubinafsisha nishati hiyo.
Amesema,ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali haina uhaba wa wataalamu wa mikataba na amebainisha kwamba,mikataba mingine wanalazimika kuingia bila kuwa na uwezo wa kujadili ikiwemo ya Benki ya Dunia.
Jaji Werema amewahi kuwa wakili wa Serikali kwa miaka 23 kuanzia mwaka 1984,na Mkurugenzi wa Katiba na Haki za Binadamu kuanzia mwaka 2007.
Anachukua nafasi ialiyoiacha Johnson Mwanyika,yupo kwenye likizo ya kustaafu kwa mujibu wa sheria.
Mwanyika aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia Desemba, mwaka 2005.
No comments:
Post a Comment