JESHI la polisi mkoani Tabora limemkamata Salum Katunija(35)kwa tuhuma za kuua watoto wanne kwa kuwachoma moto.
Katumija anatuhumiwa kuwaua watoto hao wa familia moja Oktoba 17 mwaka huu saa nne usiku.
Kwa mujibu wa Polisi watoto waliouawa ni wadogo wa mke wa mtuhumiwa, wametengana siku chache zilizopita.
Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora Emson Mmari,amesema, Katunija, anatuhumiwa kuwateketeza watoto hao katika kitongoji cha Ikami,kijiji cha Nyangahe, kata ya Bukumbi wilayani Uyui,mkoani Tabora.
Wakati watoto hao wanachomwa, mama yao mzazi,Kulwa Shija,na binti yake mwingine,Rehema Joseph,walikuwa jirani wakisherekea harusi ya ndugu yao.
Mmari amesema,wakati wakiendelea kushehereka,ghafla waliona moto ukiwaka katika nyumba yao,wakakimbia kwenda huko na kukuta nyumba hiyo ikiungua.
Amesema,walipiga kelele za kuomba msaada, wananchi wakaacha kushehereka harusi wakaenda kujaribu kuuzima moto huo lakini ilishindikana.Watoto wote waliokuwa ndani ya nyumba waliteketea.
Kwa mujibu wa Kamanda Mmari, watoto waliokufa ni Malecha Juma,(11)aliyekuwa darasa la tatu,Shija Juma,(10) aliyekuwa darasa la pili,wote walikuwa wanasoma shule ya msingi Ukili katika kata ya Bukumbi.
Marehemu wengine ni Mageta Juma,(7) na Dotto Juma (4),walikuwa hawajaanza shule. Kamanda Mmari amesema,Polisi walifanya uchunguzi wakabaini kuwa, Salum Katunija alikuwa ni mume wa Rehema Joseph,walikuwa wameachana siku chache zilizopita.
Amesema, wanandoa hao walitengana kutokana na kinachodaiwa kuwa ni mke kumchoka mume kwa sababu ya ulevi na kupigwa.
Kwa mujibu wa Mmari,Katunija alikuwa akifika nyumbani kwa mkwewe,Kulwa Shija,ili amuombe mkewe msamaha warudiane, ikashindikana.
Kamanda huyo amesema,baada ya juhudi zake kushindikana,Katunija aliamua kuwachoma moto shemeji zake kwa kuwa mkewe aligoma kurudi nyumbani.
Mmari amesema, Polisi wanachunguza kubaini ukweli wa tukio hilo,mtuhumiwa yupo rumande.
No comments:
Post a Comment