Tuesday, September 1, 2009

Kardinali Pengo na Bawaba

KUNA mdau kanitumia ujumbe huu, si vibaya nawe ukiusoma.
HAISHANGAZI kukuta gazetini au kwenye mtandao maneno yasemayo “Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini, Polycarp
Kardinali Pengo” au “The Head of the Catholic Church in Tanzania”.

Je, ni kweli Kanisa Katoliki lina wadhifa wa “ukuu wa kanisa nchini”?

Sheria ya kanisa {Can. 381(1)} inasema kila jimbo linaendeshwa na askofu wake hivyo Kardinali Pengo na uchungaji wake ni kwa Jimbo la Dar es Salaam bila kuvuka mipaka yake iliyozungukwa
na majimbo ya Morogoro, Zanzibar na Lindi.

Kinachoitwa ukuu wa kanisa nchini, hakimo katika Sheria za kanisa (Canon Laws).

Ukardinali unapodhaniwa ndiyo “ukuu” huo, basi ni ishara kuwa Kanisa Katoliki limesheheni masuala ambayo hufikia kutamkwa au kujadiliwa bila utafiti likiwemo hili la ukardinali.

Historia ya ukardinali inaambatana na Papa kuwa kiongozi wa kanisa duniani. Lakini Papa pia ni askofu wa jimbo la Roma, hivyo anahitaji wasaidizi mbalimbali.

Neno Kardinali linatokana na neno la Kilatini cardo ambalo kwa Kiswahili ni “bawaba” yaani chuma kinachoushikilia mlango ukutani kwa kupigiliwa misumari. Mlango huo asili yake ni mti uliokatwa, ukachongwa
na kutundikwa ukutani kwa bawaba.

Uhamisho wa watumishi wa kanisa kwenda jimbo jingine, ulifananishwa na ule mlango kuhamishiwa ukutani kwa
kushikiliwa na bawaba (cardo).
Hivyo zamani waliohamia jimbo lolote waliitwa “Cardinal” neno tunaloliita
“Kardinali” au “Kardinali”.

Neno “meseji” linatamkwa hata na mtoto na tunaelewa. Lakini inasisitizwa kutamka neno “ujumbe”.
Neno “Teolojia” limetamadunishwa na kuwa “tauhidi” au “taali-Mungu”.

Huwa nawaza, kwa utamadunishaji huu sitoshangaa tukiambiwa tutumie neno “ubawaba” badala ya “ukardinali” ili
iwe “Bawaba Polycarp Pengo” badala ya “Kardinali Polycarp Pengo”.
Ninavyofahamu mimi, Askofu Mkuu Pengo anatajwa kuwa ni kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini kwa sababu yeye ni Kardinali pekee Tanzania.
Kardinali Pengo ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki, Dar es Salaam, na ni raia wa Vatican.

No comments:

Post a Comment