MUDA mfupi uliopita Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imemuachia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake wanane.
Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Salum Massati, amesema, Zombe na wenzake hawana hatia kwa kuwa hakuna ushahidi kuthibitisha kuwa walishiriki kuua watu wanne Januari 14 mwaka 2006 katika msitu wa Pande, Mbezi mkoani Dar es Salaam.
Jaji Massati amesema katika hukumu hiyo kwamba, upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kwamba washitakiwa hao waliua wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi mkazi wa Dar es Salaam.
Zombe alikuwa mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, alidai kuwa alitolewa kafara kama Yesu kwa kuwa kuna watu wanamuonea wivu.
Jaji Massati amewataka polisi wakawakamate watu waliowaua wananchi hao ili washitakiwe.
Hukumu hiyo imewashangaza watu waliokuwa mahakamani na walionekana kutoamini alichokisema Jaji huyo.
Jaji Massati amesema, upande wa mashitaka unaweza kuwasilisha pingamizi la hukumu hiyo katika kipindi cha siku 14 kuanzia leo.
Alisoma hukumu hiyo kwa takribani saa sita katika chumba namba moja katika Mahakama Kuu Tanzania, Dar es Salaam.
Kabla ya kusoma hukumu hiyo Jaji Massati alisoma muhtasari wa mashahidi 37 waliotoa ushahidi katika kesi hiyo iliyoanza mwaka 2006.
No comments:
Post a Comment