Taarifa ya Kamati hiyo maalum, kwa mujibu wa gazeti la Tanzania Daima la tarehe 26 Mei, 2009 inanitaka nisitoe kauli zisizo za kitaalamu! Nina maswali kadhaa ya kuuliza:
Kwanza, ni utaalamu gani unahitajika kuelezea kitu kilichomsibu mtu?
Mathalan, nyumba yangu imeungua moto. Kwa mantiki ya kamati hiyo maalum, siruhusiwi kuelezea kuwa chanzo cha moto kilikuwa kibatali au mshumaa, mpaka nimsubiri Kombe na timu yake ya “wataalam” waje kupiga ramli kama walivyofanya kwenye ajali yangu?
Pili, tumepata ajali nyingi nchini na abiria na madereva wamekuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa Polisi kujua chanzo cha ajali.
Kwa nini vigezo na taratibu zigeuke kwenye ajali ya Dk. Mwakyembe peke yake (ambapo wahusika wakuu katika ajali hiyo hawatakiwi kuongea)?
Tatu, kama suala hapa ni uelewa wa sheria husika, mwenendo wa upelelezi na wa mashitaka, ni nani katika Kamati hiyo ya Kombe anayeweza akadai kuwa na uelewa mpana na wa kina kunipita?
Tumepata ajali nyingi kama Taifa zilizosababisha majeraha na vifo vya wananchi na viongozi na hata kuzua maswali mengi kuhusu vyanzo vya ajali hizo bila Polisi kuingilia uhuru wa kusema wa majeruhi wala kuunda Kamati maalum za uchunguzi.
Lakini ajali yangu ambayo kwa ulinzi na baraka za Mwenyezi Mungu haijasababisha upotevu wa maisha, inajengewa kwa makusudi mazingira ya malumbano na kuundiwa Kamati maalum ya uchunguzi yenye lengo la kuziba watu midomo.
Hamasa hii ya Jeshi la Polisi kudodosa kila ninalolisema na kulitafutia maelezo mbadala, inatokana na nini, inachochewa na nini na kwa faida ya nani?
Kwa kuwa sheria za nchi zinataka vyombo vya kiutawala vya maamuzi (quasi-judicial bodies) vizingatie kanuni za haki za asili (principles of natural justice), ni nini kiliizuia Kamati hiyo maalum kunihoji mimi na dereva wangu ili kukidhi matakwa ya kanuni za haki za asili na kupata picha iliyo kamilifu zaidi ya ajali hiyo?
No comments:
Post a Comment