GHARAMA za kuhifadhi zaidi ya tani 290 za samaki waliokamatwa katika meli ya uvuvi, MV Tawariq1, kwenye bahari ya Hindi eneo la Tanzania zimefika zaidi ya sh bilioni moja.
Samaki hao waitwao Jodari wana thamani ya sh bilioni mbili na hadi sasa haijulikani watauzwa lini.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Jonas Melewasi amesema, kwa kuwa mahakama iliagiza samaki hao wauzwe kwa mnada, mchakato wa kuwapata watakaosimamia uuzwaji huo unaendelea.
Alikiri kuwa kuchelewa kuwauza samaki hao kunaongeza gharama za kuwahifadhi samaki hao katika kampuni ya Bahari Foods Limited ya Dar es Salaam.
Hadi sasa haifahamiki samaki hao wapo chini ya Wizara au polisi, kwa kuwa Ijumaa iliyopita , Msemaji Mkuu wa Wizara hiyo, Judith Mhina, alisema, wapo chini ya polisi na wanaisubiri mamlaka hiyo itangaze mnada ndipo wao (Wizara) watakachukua jukumu la kusimamia uuzwaji.
Mhina alisema, kwa kuwa wapo chini ya uangalizi wa polisi ni jukumu la mamlaka hiyo kusema mnada utafanyika lini na wapi, na kwamba Wizara itasimamia mnada huo.
Kaimu Mkurugenzi wa Upepelezi Makosa ya Jinai, Peter Kivuyo amesema si kweli kuwa samaki hao wapo chini ya Polisi, wapo chini ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Aprili saba mwaka huu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ilikubali ombi la upande wa mashitaka la kutaka samaki hao wauzwe kwa mnada na fedha zitakazopatikana ziwekwe kwenye mfuko maalumu wa serikali kama kielelezo mahakamani.
No comments:
Post a Comment