Monday, April 27, 2009

Ni huduma au biashara?

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili inatoza sh 20,000 kila siku kuhifadhi maiti katika chumba cha maiti hospitalini hapo, sh 30,000 kuweka dawa kwenye mwili wa marehemu Mtanzania, sh 200,000 kufanya uchunguzi wa mwili wa raia wa Tanzania na sh 25,000 kuosha na kuuvisha mwili.

Maiti ambao si raia wa Tanzania wanalipiwa sh 60,000 ili kuwekewa dawa, na sh 400,000 kufanyiwa uchunguzi.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Muhimbili, Aminiel Algaesha amesema, viwango hivyo si vikubwa, na vinalingana na ubora wa huduma hizo katika chumba za kuhifadhia maiti hospitalini hapo.

“Hizi ndiyo gharama zetu tulizoweka ili kukidhi mahitaji” alisema Algaesha na kubainisha kwamba, uongozi wa hospitali umeweka gharama hizo ili wafiwa wasiache maiti zikae muda mrefu Muhimbili.

Kwa mujibu wa Algaesha, wafiwa wanatozwa fedha hizo ili pia kufidia gharama za uendeshaji kwa kuwa chumba cha kuhifadhia maiti Muhimbili kina majokofu ya kisasa yanayotumia umeme mwingi.

Alisema Muhimbili haiwakomoi watu na kusema gharama za kuhifadhi maiti na huduma nyingine kwa marehemu Muhimbili ni ‘standard’ hasa ikizingatiwa kuwa ni hospitali ya rufaa.

Mtu akifariki dunia Muhimbili na mwili wake kuhifadhiwa katika chumba cha maiti hospitalini hapo, kuanzia siku ya tatu wafiwa watatozwa sh 20,000 kila siku utakazohifadhiwa, na endapo maiti itatoka nje ya hospitali hiyo kwenda kuhifadhiwa hapo wafiwa watatozwa kiasi hicho kuanzia siku mwili utakapofikishwa.

No comments:

Post a Comment