Friday, July 26, 2013

Mke aliyetaka kumuua mumewe, mtoto kizimbani

 MKE wa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha , Janeth Jackson (32) anayedaiwa kupanga njama za kumuua mumewe wa ndoa na mtoto wa mume huyo, amepandishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha pamoja na mtuhumiwa mwingine.

Janeth ambaye ni mkazi wa Moshono jijini Arusha pamoja na Novatus Elias walifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha /Arumeru, Devotha Kamuzora wakisomewa makosa mawili ya kula njama ya kutaka kumwua Jacksoni Manjuru .

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Edna Kasala alidai mahakamani hapo kuwa washitakiwa wote wawili walitenda kosa la pili la kula njama na kutaka kumwua Desderi Sabas ambaye ni mtoto wa nje wa mume huyo anayeishi Bukoba mkoani Kagera.

Washitakiwa wote hawakutakiwa kujibu lolote mahakamani hapo kwa sababu Mahakama hiyo kisheria haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Mwendesha Mashitaka huyo wa Serikali aliiomba Mahakama kuwanyima dhamana watuhumiwa kwa sababu watuhumiwa wengine wawili katika kesi hiyo wanatafutwa na hivyo kudai kutoa dhamana kunaweza kuharibu upelelezi ambao haujakamilika.

Alidai kutokana na uzito wa tuhuma hizo maombi hayo ya kuwanyima dhamana watuhumiwa yameambatanishwa na hati ya kiapo ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani Arusha.
 
“Mheshimiwa tunafahamu kwamba dhamana ni haki ya washtakiwa kikatiba lakini kutokana na mazingira ya kesi hii kuwa magumu tunaomba dhamana isitolewe ili kuwatafuta watuhumiwa wengine wa kesi hii,” alidai mwendesha mashitaka.
 
Wakili wa Utetezi, Fidelis Peter alipinga maombi hayo na kutaka Mahakama itoe dhamana kwa washitakiwa kwa sababu ni haki yao ya kikatiba na kuwa hilo lilikuwa kosa lao la kwanza.
 
Alitoa sababu nyingine ya kupinga maombi ya upande wa mashitaka kwamba sababu kuwa watuhumiwa wanaweza kuvuruga upepelezi wakiachiwa kuwa si za msingi kwa kuwa ni watu wanaoaminika katika jamii.
 
“Mheshimiwa sababu za kuwanyima dhamana watuhumiwa hazina uzito wowote pia mshitakiwa wa kwanza (Janeth) ana mtoto wa miezi sita na tangu akamatwe Alhamisi iliyopita hajamwona wala kumnyonyesha mwanawe hivyo anastahili kupewa dhamana,” alidai Peter.

Baada ya kusikiliza maombi ya pande zote, Hakimu Kamuzora alikubaliana na maombi ya upande wa mashitaka na kuamuru watuhumiwa warejeshwe ndani hadi Agosti 5, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Chanzo: Habarileo

No comments:

Post a Comment