Tuesday, May 14, 2013

Ni kweli?


Kuna madai kuwa, kuna wabunge wawili katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamejazwa mimba na wabunge wenzao.
 
Awali, kulikuwa na uvumi kuwa mmoja wa wabunge wa upinzani (Viti Maalum), akitoka Kanda ya Kaskazini, amepewa ujauzito na mheshimiwa mwingine ambaye ni kiongozi anayeshika nafasi za juu kwenye moja ya vyama vikuu vya upinzani nchini (wote majina yao tunayahifadhi kwa sasa).
 
Kashfa hiyo ya mtunga sheria huyo kupewa mimba na mheshimiwa mwenzake ambaye ni mume wa mtu, ilipata mbeleko na kuifanya ivume zaidi, baada ya Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, kulipuka bungeni:
 
 “Humuhumu ndani kuna wabunge wanawake wenye mimba zisizotarajiwa.”

Lusinde, alitamka hayo Aprili, mwaka huu, wakati akichangia hotuba ya bajeti, Ofisi ya Waziri Mkuu, kipindi ambacho bunge lilikuwa limechafuka kutokana na wabunge kurushiana ‘mipasho’ wao kwa wao.

Kauli ya Lusinde, pamoja na kupokelewa tofauti na wabunge wengi wanawake, wakidai mheshimiwa mwenzao amewadhalilisha, upande mwingine, katika ‘vikao vya kwenye korido’, matukio ya vicheko na kugonga mikono yalitawala na kunena kwa msisitizo “message delivered”, yaani ujumbe umefika.

Wakati mwandishi wetu akifuatilia sakata lenyewe, mbunge mwingine wa Viti Maalum (CCM) ambaye jina lake tunaliweka kabatini, aliamua kufunguka: 
 
“Nashangazwa sana na haya madai, tunawasema wapinzani, wakati hata kwetu (CCM) kuna watu wamepeana mimba.”
 
Mbunge huyo alisema kuwa siyo siri mjengoni kuwa mmoja wa watunga sheria wa CCM, anayetokea moja ya majimbo ya Kanda ya Magharibi, amempa ujauzito mheshimiwa mwingine kutoka chama tawala, anayewakilisha viti maalum (majina yao yamehifadhiwa kabatini kwa sasa).
 
Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, mbunge anayetajwa kupewa mimba, anatokea kwenye ukoo wa mmoja wa vigogo waliowahi kushika nafasi za juu kabisa kwenye Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Wabunge mbalimbali waliozungumza na mwandishi wetu, walikiri kutambua uwepo wa wenzao wenye uhusiano wa kimapenzi kiasi cha kufikia kupeana mimba.
Mbunge mwingine alithubutu kutamka: “Nini hao kupewa mimba na zinaonekana, wapo ambao wanapata na wanatoa. Yote hayo tunayajua.”

Katika kufanyia kazi kila kinachozungumzwa, mwandishi wetu alizungumza na baadhi ya wabunge ambapo Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, alisema: Unajua madai ya mimba yanawahusu wanawake, kwa hiyo waulizwe wenyewe.
“Kama umenitafuta mimi kwa kigezo kwamba ni mbunge kijana, basi waulize wabunge vijana wanawake,” alisema Mnyika.
 
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alikiri kufahamu kuwepo kwa tuhuma kwamba wapo wabunge wamepeana mimba lakini hawezi kuwa na uhakika kwa sababu uhusiano wa kimapenzi ni jambo la faragha.
 
“Hayo madai yapo, yanazungumzwa. Wapo wanaotajwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi, hayo ni mambo ya faragha. Sijui pengine walioanzisha haya madai wana vipimo vyao,” alisema Kafulila. 

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Morogoro, Sara Msafiri, alisema kuwa haiwezekani wabunge kupata mimba zisizotarajiwa kwa sababu ni watu wazima.
“Wabunge tunapata mafunzo ya uzazi, kwa hiyo kama ni mimba basi mtu anakuwa amepanga kuipata. Hakuna  kitu kama hicho. Hata hilo la kutoa mimba halipo kabisa, sijawahi kusikia mtu amefanya hivyo bungeni,” alisema Sara.


Kwa upande wa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Grace Sindato Kiwelu, alisema: “Sitegemei upande huo wa wabunge kupata mimba zisizotarajiwa, kwani wanaofanya mapenzi ni watu wazima hivyo wanafanya wakijua kwamba wanatarajia kupata nini.”
 
Mbunge mwingine wa Viti Maalum (Chadema), Chiku Abwao, alisema: “Hakuna mbunge anayepata mimba isiyotarajiwa, kwanza nilimshangaa mbunge kutamka mambo kama hayo, alistahili kuwaambia watoto, lengo lake lilikuwa kudhalilisha wanawake.”
 
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Munde Tambwe, alisema: “Ile kauli ya Lusinde kwamba kuna wabunge wanapata mimba zisizotarajiwa, nadhani kuna mtu alikuwa anamlenga, kwa hiyo mimi siwezi kulizungumzia.”

No comments:

Post a Comment