Mfanyabiashara maarufu katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha Joseph Sambeke (49) maarufu kama Bob Sambeke amekufa.
Bob Sambeke
alianguka na ndege ndogo juzi jioni kilomita moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Arusha wakati
akitoka mkoani Kilimanjaro.
Ndege ya
Sambeke aina ya MT 7- namba 5H-QTT ilianguka saa 12.34 jioni baada ya
bawa lake kugonga mti katika eneo la Magereza linalopakana na uwanja
huo.
Alijeruhiwa na baadaye aliaga dunia akiwa njiani wakati akiwahishwa
hospitalini na askari wa Magereza ambao wanaishi katika kambi
alipoanguka.
Mazishi yake yamepangwa kufanyika Alhamisi eneo la Karanga,
Moshi.
Meneja wa Uwanja wa Ndege Arusha, Ester Dede amesema taarifa za awali zinaonyesha
ndege hiyo ni mali ya marehemu Mawalla ambaye alikuwa mbia wa biashara
na Bob Sambeki na imesajiliwa kupitia Kampuni ya Quality Tours &
Travellers.
Wakili Alex Msando, ambaye pia alikuwa mshirika
wa Mawalla, aliliambia gazeti hili kuwa Sambeke alikuwa ameinunua ndege
hiyo kutoka kwa marehemu.
Dede alisema, ndege hiyo
ikiongozwa na rubani Bob Sambeki ina uwezo wa kubeba watu wanne akiwamo
rubani. Baadhi ya walioshuhudia tukio hilo, walisema kabla ya kuanguka
ndege hiyo, ilikuwa ikiyumba na iligonga mti mkubwa katika moja ya
mabawa yake na kupoteza mwelekeo.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Julias Laizer alisema, aliona
ndege hiyo ikigonga mti na kuyumba, kisha kudondoka chini na ndipo
askari wa magereza walipojitokeza kutoa msaada. Laizer alisema Sambeki
alikuwa peke yake na alijeruhiwa kichwani.

No comments:
Post a Comment