Sunday, October 14, 2012

Walivyomuua RPC Mwanza

Na Sitta Tumma, Mwanza

MAUAJI ya kinyama ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, yaliyotokea usiku wa kuamkia jana, yamelishitua taifa.

 Hili ndilo geti la nyumba anayoishi Mwalimu Doroth Moses, katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza.
Pembeni ya geti hilo ndipo alipouawa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow.

 Nyumba ya Mwalimu Doroth Moses wa shule ya Msingi ya Nyamagana ambye alikuwa kwenye gari aina ya Toyota Rav 4 aliyokuwa akiendesha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow usiku wa kuamkia Jumamosi.

Kamanda Barlow aliuawa majira kati ya saa sita na saba usiku na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na kusababisha Jiji la Mwanza kuzizima kwa simanzi.

 Kamanda Liberatus Barlow

Barlow ambaye ni mmoja kati ya makamanda wanaojulikana sana nchini kutokana na changamoto zilizopo kwenye mikoa yao, aliuawa kwa kumiminiwa risasi zisizo na idadi shingoni na kusababisha kifo chake papo hapo.

Inaelezwa kuwa kamanda huyo alishambuliwa majira ya kati ya saa saba na nane usiku katika eneo la Kitangiri karibu na Hoteli ya Tai Five, iliyoko barabara ya Kona ya Bwiru jijini Mwanza  wakati akitoka kwenye kikao cha harusi.



Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lily Matola, alisema mauaji hayo ya kinyama dhidi ya Kamanda Barlow yalitekelezwa na kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na walimfyatulia risasi ambazo hadi sasa idadi yake haijajulikana.

                   Waombolezaji nyumbani kwa Kamanda Liberatus Barlow.
Alisema ingawa bado hawajafahamu idadi hasa ya risasi alizopigwa na kusababisha kifo chake, tayari Jeshi la Polisi nchini limeshaanza kufanya uchunguzi wa kina na wa kitaalamu kubaini na hatimaye kuwakamata waliohusika.
Kabla ya kuawa alitoka wapi?
Kabla ya Kamanda Barlow kufikwa na mauti, inadaiwa alikwenda kushiriki kikao cha harusi ya mtoto wa dada yake aliyetajwa kwa jina la Sembeli Mareto, kilichofanyika katika hoteli ya Florida, iliyopo eneo la Kitangiri na kikao hicho kilimalizika majira kati ya saa nne na sita usiku.

 Mtoto wa kaka yake Mwalimu Doroth Moses akiongea kuhusiana na tukio la kifo cha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow.
Mtoto huyo ndiye aliyefungua geti usiku ili Mwalimu huyo aingie ndani, wakati anafanya hibyo akasikia risasi zilizomuua kiongozi huyo mkuu wa polisi Mwanza.
                                Nyumbani kwa marehemu Kamanda Liberatus Barlow.
“Ni kweli kamanda wetu wa Polisi Liberatus Barlow amefariki dunia kwa kupigwa risasi za moto. Ni tukio kubwa sana na la kinyama! Haijafahamika alipigwa risasi ngapi hadi kufariki dunia papo hapo.Tayari upelelezi wa kina umeshaanza. Na tutahakikisha wote waliohusika katika shambulizi hilo wanakamatwa,” alisema. 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Injinia Everestine Ndikilo, alisema jana kuwa taarifa za awali zinaonesha kuwa Kamanda Barlow alipigwa risasi sehemu za bega na kutokezea upande wa pili wa shingo akiwa kwenye gari lake binafsi, aina ya Toyota. 

Mwanamke aliyekuwa naye ashikiliwa Polisi
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo, Injinia Evarist Ndikilo, aliwaeleza waandishi wa habari ofisini kwake kwamba, mauaji hayo dhidi ya kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, kamwe hayavumiliki.

 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Everest Ndikillo


Kwa mujibu wa habari hizo, baada ya kuona hali hiyo, mwanamke huyo alimuuliza Kamanda Barlow kama anawafahamu watu hao.

“Baada ya mwanamke huyo kumuuliza RPC kama anawafahamu watu hao, alisema anaona kama ni walinzi wa Jamii. 

Wakiwa bado wanaulizana wale watu walizidi kulisogelea gari huku wakisema ‘kwa nini mnatuwashia mwanga mkali na gari lenu’?

“Wakati watu hao wakiuliza hivyo huku wakiwa wanalisogelea gari la RPC, Barlow, aliwauliza ‘mimi hamnijui’?”  alisema Ndikilo.
Habari zinasema kuwa wakati mama huyo anateremka kutoka kwenye gari hilo, watu wengine kama watatu walilisogelea gari la Kamanda Barlow.

Kuona hivyo, Kamada Barlow alichukua radio call aliyokuwa nayo ili kuwasiliana na askari wake, lakini watu hao walilivamia gari lake na kuanza kumshambulia kwa risasi.

“Wakati anashika redio yake ili awasiliane na askari wake, idadi ya watu kama watano hivi walifika eneo hilo wakampiga risasi za begani na kutokezea sehemu za shingoni na baada ya shambulio hilo, kamanda wetu akawa amepoteza maisha papo hapo, wala hakuweza kupambana na wahalifu hao,” alisema Ndikilo.

Inaelezwa kuwa baada ya shambulio hilo lililodumu kwa sekunde kadhaa, damu nyingi zilimwagika na watu hao wakakimbia na radio call hiyo pamoja na simu mbili za marehemu na pochi ya mwanamke aliyekuwa naye iliyokuwa na fedha ambazo kiasi chake hadi sasa hakijajulikana.

Mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na kuongeza kuwa jeshi hilo Makao Makuu jijini Dar es Salaam, limemtuma DCI Manumba kuongoza upelelezi wa kina kubaini wahusika.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza, aliiitaka jamii na wakazi wa Mwanza kuwa na subira kipindi hiki cha majonzi katika kuwasaka wahusika wa tukio hilo.
Tetesi za mitaani
Tetesi za mitaani zinaeleza kwamba, tukio la kuuawa kwa Kamanda huyo huenda limesababishwa na uhasama na watu mbalimbali katika maeneo ya kazi alikowahi kufanya na kwamba hilo ni tukio linalotia shaka kama imetokea kwa bahati mbaya.

Baadhi ya watu wanalihusisha tukio hilo na mahusiano ya kimapenzi, misimamo yake mikali ya kupambana na majambazi, ambapo alikuwa akitoa onyo kwa majambazi kutoingia katika eneo lake la kazi.
Watoto wa Doroth wana siri nzito
Kwa upande wao, watoto wa Doroth Moses walisema kwamba siku ya tukio mama yao aliwaaga jioni kuwa anakwenda katika kikao cha harusi cha rafiki yake maeneo ya Florida Hotel na wakati anarudi nyumbani majira ya saa 4 usiku aliwapigia simu ili wamfungulie geti.

 Mwalimu Doroth Moses aliyekuwa na Rpc Barlow 
 
Walisema wakati mtoto mmoja, Keny Rogers (17), akienda kumfungulia geti, aliona kundi la watu kama watano wakiwa wamezunguka gari la Kamanda Barlow.

“Yule mwanaume (RPC), aliyekuwa amemleta mama (Doroth), sisi hapa hatumjui na hata hatujawai kumuona. Lakini mama alitupigia simu akisema tumfungulie geti.

“Wakati mimi nimeenda kumfungulia geti, niliona kundi la watu watano lakini mimi hawakuniona. Wakati naendelea kuwacheki (kuwaangalia), kama nawafahamu ama la, ghafla nikasikia mlio wa bunduki kisha wale watu wakakimbia. Nikaanza kuona damu nyingi zinamwagika chini,” alisema mtoto Keny.

Picha za msibani kwa hisani ya blog za mikoa

No comments:

Post a Comment