Sophia Simba akiingia katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Cha Mipango, Dodoma Oktoba 20,2012 kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa UWT. Katika uchaguzi huo, Waziri Simba alishinda.
Raia Mwema: Wasomaji wetu wangependa kukufahamu kwa sababu mengi yamekuwa yakisemwa na yakinong’onwa hususan kuhusu elimu yako; labda kwa vile hawaifahamu vizuri. Unaweza kutupa CV yako kwa kifupi?
Mama Sophia Simba: Asante kwa kunipa nafasi hii
adimu. Nimefurahi kwamba umeweza kufika ofisini kwangu na kuweza
kuongea na mimi. Nashukuru kwamba umeona upo umuhimu wa watu kunijua
mimi Sophia ni nani hasa.
Ni kweli maneno mengi yamekuwa yakisemwa ambayo hayapendezi, lakini
nitafanyaje? Kwa hiyo, kwa kifupi sana ningependa nikufahamishe
labda pengine kwa kupitia wewe watu watanifahamu.
Mimi naitwa Sophia Simba. Ni Sophia Mathew Simba. Nyambi ni jina
langu la nyumbani. Wazaramo wana majina yao ya ukoo, kwa hiyo mimi ni
Nyambi na mdogo wangu alipewa jina lingine. Nilipokuwa mdogo baba
yangu akasema huyu ni Nyambi.
Kwa kifupi sana, mimi ni mtoto wa mfanyabiashara. Baba yangu
alitokea Kisarawe, kijiji kinachoitwa Sungwi. Baba yangu alisoma
Minaki. Alipomaliza Minaki alirudi hapa Dar es salaam. Baba yangu
aliwahi kufanya kazi mpaka ya uvuvi. Aliacha shule kutokana na umbali
kutoka kijijini kwake Sungwi kwenda Minaki.
Watoto waliokuwa wakitoka bara walikuwa wanasoma boarding, lakini
watoto wa Kisarawe wenyewe walikuwa wanatakiwa watembee umbali mrefu.
Kwa hiyo, kutokana na hiyo alifikia mahali haikuwezekana.
Baba yangu mwanzoni alikuwa Mwislamu.
Alikuwa anaitwa Omari Simba.
Kutokana na kusoma pale Minaki, aliamua kubadilisha dini. Baba yangu
alibatizwa katika Kanisa la St. Albans – hili la hapa mjini. Na baada
ya hapo baba yangu aliondoka akaenda Morogoro kufanya shughuli za
biashara.
Kule alikutana na mama yangu, mwanamke wa Kiluguru ambaye naye
historia yake alikuwa Sister wa Roman Catholic. Kwa hiyo walikutana na
wakaoana.
Katika maisha yetu yote tumeishi kama Wakristu wa Roman Catholic.
Mpaka leo mimi ni Mroman Catholic ingawaje kila mtu ananipa dini
ambayo anaitaka. Kwa hiyo, mimi ni mmoja wa watoto tisa. Mimi ni wa
pili.
Raia Mwema: Makazi yenu hasa yalikuwa wapi?
Mama Sophia Simba: Makazi yetu yalikuwa Dar es
salaam na Morogoro. Dar es Salaam tuliishi Bungoni, Ilala. Lakini
tukiwa wadogo kabisa baba yangu alijenga nyumba yake ya kwanza kabisa
Morogoro, Kwa Kingu.
Alifanikiwa sana kwa shughuli za baa. Mimi ni mtoto ambaye
nimesomeshwa kwa pesa za pombe. Baba yangu alikuwa na baa inayoitwa
Uzaramo Bar, Morogoro lakini pia alikuwa na baa inayoitwa Simba Bar.
Kwa hiyo, mimi kufungua vizibo vya bia najua.
Nikiwa bado mdogo nilikuwa nauza mishikaki. Siku zote nyumba yetu
ilikuwa upande baa, upande tunaishi sisi. Kwa hiyo, baba yangu
aliendelea na shughuli za baa muda mrefu.
Raia Mwema: Ulianza shule wapi?
Mama Sophia Simba: Mimi nilianza shule Morogoro
katika shule inayoitwa Kilakala, baada ya hapo nikapelekwa shule ya
boarding inayoitwa Ilonga Middle School, Kilosa. Baada ya hapo
nikasoma Forest Hill Secondary School. Sisi ndiyo waanzilishi wake.
Ule mwaka ambao wanafunzi wengi tuliambiwa hatukuchaguliwa
tuliunganishwa darasa la saba na la nane. Kwa hiyo sisi tulimalizia
darasa la nane. Huo ulikuwa mwaka 1965. Shule nyingi (za binafsi)
zilianzishwa mwaka huo. Shule za Kibohehe, Forest Hill, Mzizima na
Kinondoni, zote zilianza wakati huo.
Baada ya pale nikaenda Kibosho Secondary School. Kwa bahati mbaya
baba akafariki, wakati huo nikiwa nafanya kazi NDC. Kabla hajafariki,
baba alitaka sana nifanye shughuli za biashara, niendeleze biashara ya
familia.
Baada ya kumaliza shule nilichaguliwa nikasomee ualimu lakini
sikwenda, na badala yake nikapata kazi NDC. Hapo NDC nilianza kazi
1971 hadi mwaka 1979.
Baada ya hapo nikaingia Lonrho Group of Companies baada ya kuacha
kazi NDC. Kutoka pale nikaanza kazi Metal Engineering Industries
Development Association (MEIDA) ambayo ilianzishwa na Waswedish.
Nikiwa hapo nikaamua kwenda kusoma. Nilianza mafunzo ya Certificate of
law mwaka 1985. Nilipenda sana kusomea sheria.
Mwaka 1987 nilianza kusomea shahada ya sheria katika Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, na nikahitimu mwaka 1992 au 1993. Kuna mwaka hapo
katikati chuo kilifungwa kwa sababu ya kuwapo mgomo.
Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu nikarudi kufanya kazi Metal Industries;
kwani wakati nasoma walikuwa wamenipatia likizo isiyokuwa na malipo.
Baada ya kurudi walinipandisha cheo kuwa legal and administrative
officer; kwani kabla ya kwenda chuo kikuu cheo changu kilikuwa
administrative officer tu.
Wakati niko NDC nilikuwa katibu wa tawi la UWT la NDC na Mama Anna
Mkapa alikuwa mwenyekiti wetu, tulifanya mambo mengi mazuri.
Nilipokuwa MEIDA niliomba pia kuwa diwani wa viti maalumu. Kulikuwa
na uchaguzi mwaka 1993 au 1994. Nikawa diwani hadi 1995. Mwaka 1995
wakasema kuna viti maalumu vya ubunge kwa akina mama. Mimi nikagombea
vitu maalumu.
Mwaka huo wa 1995 nilipata invitation ya kwenda Beijing, China
kuhudhuria mkutano wa wanawake duniani. Nikakataa, nikampa mwenzangu
nikamwambia mimi siendi nitabaki hapa kwa ajili ya kampeni za ubunge.
Sikwenda mimi Beijing kwa sababu ya kampeni hiyo. Kwa hiyo mwaka 1995
Nikashinda, na hivyo nikaingia bungeni.
Mwaka 1995 nilifanya mafunzo ya Post Graduate Diploma on Women Law
kwenye Chuo Kikuu cha Zimbabwe na mwaka 2005 nilifanya Masters ya
Community Economic kwenye Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Thesis yangu
ilikuwa Women and Economic Empowerment in Tanzania.
Mwaka 1972 mimi niliolewa. Mume wangu alikuwa ni mwanasheria wa
Chama cha Ukombozi cha Afrika Kusini cha ANC. Siku zile walikuwa
wakiwaita wakimbizi, lakini wenyewe walikuwa wanataka waitwe freedom
fighters.
Mume wangu aliruhusiwa pia kufanya kazi za uanasheria nchini. Kabla
ya kufariki aliwahi kufanya kazi pia benki. Alikuwa anaitwa Clifford
Zex Senge. Wengi walikuwa wanamwita kwa jina la Cliff. Wanasheria
wengi wanamjua.
Kwa hiyo, niliolewa na Cliff na nikazaa naye watoto wawili. Watoto
hao walikwenda Afrika Kusini kwa baba yao lakini sasa wote wamerudi.
Maisha ya Afrika Kusini ni magumu hayako that easy.
Kuna watu wanasema mimi ni kituo cha polisi, wanaume wananikimbia.
Nilisoma kwenye gazeti (eti) wanaume hawanitaki. Lakini I was married.
Raia Mwema: Uliolewa na Msouth Afrika na kwa bahati
mbaya akafariki dunia. Lakini nasikia ulikuwa na mahusiano na
ulionekana mwaka 1995 ukiwa na Kitwana Kondo, Meya wa zamani wa Dar
es Salaam na mbunge wa zamani wa Ilala. Uhusiano wako na yeye ulikuwa
wa aina gani?
Mama Sophia Simba: Sawa, mimi nilikutana na Mzee
Kondo… Kwanza nakubali nilikuwa na mahusiano naye, na nimezaa naye
mtoto wa kiume. Nilikuwa na Mzee Kondo kutoka mwaka 1975. Nilikutana
naye wakati akigombea ubunge; mimi nikiwa kama mpiga debe wake. Kwa
hiyo tulikutana mwaka 1975 na tukaachana mwaka 1983.
Siyo kama tulioana, hapana, alikuwa boyfriend. Yeye siku zote
amekuwa na mke wake. Kwa hiyo, nilizaa naye kweli mtoto mmoja na mpaka
sasa hivi mimi namuheshimu Mzee Kondo. Na baada ya hapo, mwaka 1983,
ameshaoa mara mbili au mara tatu lakini mimi bado namheshimu mpaka
watu hawaelewi mahusiano yangu mimi na yeye yakoje.
Hata tulipokwenda bungeni watu wengine walidhania ni mtu na mkewe,
lakini mimi sijaolewa na Kitwana Kondo. Namheshimu sana, ni baba wa
mtoto wangu.
Raia Mwema, Tanzaniteglamour
hongera sana mama simba.umetoa ukweli wako maana wengine huwa wanajikosha.
ReplyDelete