Mbunge wa Bahi (CCM) mkoani Dodoma, Omary Ahmed Badwel akishuka katika gari wakati alipofikishwa katika Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam leo.
Mbunge wa Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel akielekea katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
Mbunge wa Bahi (CCM), Omary
Ahmed Badwel akiwa chini ya ulinzi wakati akitoka Mahakamani baada ya kusomewa shitaka la rushwa ya sh. milioni moja kutoka kwa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana.
Picha zote na www.francisdande.blogspot.com
MBUNGE
wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel (43) leo amefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam,na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa(Takukuru), kwa makosa ya kupokea rushwa ya shilingi milioni
moja kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan
Liana.
Wakili
wa Takukuru, Janeth Machullia na Ben Lincoln walidai mbele ya Hakimu
Mkazi Faisal Kahamba kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili ya
rushwa.
Wakili Machullia alidai kuwa kosa la kwanza ni la rushwa
kinyume na kifungu cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa Na.11 ya mwaka 2007, kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka huu
katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam , Badwel akiwa ni Mbunge wa
Bahi na Mjumbe Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) na wakati huo
akiwa ni ofisa wa serikali kwa maana ya sheria ya Takukuru, alitenda
kosa la kushawishi ili apewe rushwa ya jumla ya Shilingi milioni nane
toka kwa Liana ili aweze kuwapelekea
wajumbe wenzake wa Kamati hiyo ya Bunge ili waweze kuipitisha ripoti ya
fedha ya mwaka 2011/2012 ya Halmashauri hiyo.
Wakili
Machullia alidai kuwa, shitaka la pili ni kwamba kati ya Juni 2 mwaka huu,
katika Hoteli ya Peacock, mshitakiwa akiwa na nyadhifa zake zote hizo
alipokea rushwa ya milioni moja kutoka kwa Liana ili aweze kwenda
kuwashawishi wajumbe wa Kamati hiyo ili waweze kuipitisha ripoti ya
fedha ya Halmashauri ya Mkuranga huku akijua kufanya hivyo ni kosa.
Hata
hivyo mshitakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki
alikanusha mashitaka yote na wakili wa Machullia alidai kuwa upelelezi
wa shauri hilo umekamilika.

No comments:
Post a Comment