Mwenyekiti wa CCM, Jakaya kikwete (kulia) akiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya TaifaItikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
TAMKO LA NEC KUHUSU KUKOMESHA TATIZO LA RUSHWA KWENYE UCHAGUZI NDANI YA CHAMA
Kikao
cha NEC baada ya kujadili kwa kina changamoto zinazokikabili Chama Cha
Mapinduzi wakati wa uchaguzi wa ndani ya Chama kimebaini tishio la tatizo la rushwa. Hivyo NEC imesisitiza kusimamia kwa ukamilifu ahadi ya Mwanachama wa CCM inayosema;
“Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa”,
Na pia kusimamia kwa nguvu zaidi Kanuni za Chama za Uchaguzi Na.33(2) inayosema:-
"Ni
mwiko kwa kiongozi mgombea au mwana-CCM kutoa au kupokea rushwa. Kwa
ajili hiyo, Kiongozi, mgombea yeyote wakati wa uchaguzi akithibitika
kuwa ametumia rushwa katika jitihada zake za kuwania nafasi anayoiomba
hatateuliwa kugombea nafasi hiyo.
Hali
kadhalika, mgombea yeyote atakayethibitika kuwa ameshinda uchaguzi kwa
njia ya kutoa rushwa, atanyang’anywa ushindi alioupata, na pia atazuiwa
asigombee tena katika uchaguzi mwingine wowote kwa muda utakaoamuliwa na
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa; au atapewa adhabu kubwa zaidi
ya hiyo kama itakavyoonekana inafaa."
Hivyo basi NEC imetoa maagizo yafuatayo:-
(a)
Kuanzia sasa ni marufuku kwa mgombea wa ngazi yoyote kuzunguka
matawini, kwenye kata, wilayani na mikoani kukutana na Wajumbe wa
mkutano utakaomchagua kwa kisingizio cha kuwasalimu Wajumbe,kuwapa nauli
au kujitambulisha.
Mgombea atakayethibitika anazunguka/ amezunguka
ataondolewa bila kuchelewa katika orodha ya wagombea.
(b) Kwa watendaji na viongozi wa Chama wa ngazi zote kuanzia sasa ni marufuku kuwatembeza wagombea ndani ya maeneo yao
kwa nia ya kuwatambulisha kwa wapiga kura.
Mtendaji/kiongozi
atakayebainika anakiuka agizo hili atachukuliwa hatua za kinidhamu mara
moja.
(c)
Kuanzia sasa ni marufuku kwa watendaji na viongozi wa Chama wa
ngazi zote kuwaitia wagombea Wajumbe wa mikutano ya Uchaguzi kwa lengo
lolote lile, kwani vikao vya aina hiyo havimo katika Katiba, na ni vikao
haramu vinavyopalilia rushwa.
NEC
imetoa wito kwa wana-CCM popote walipo wapige vita rushwa na watoe
taarifa ya vitendo vya rushwa katika Ofisi za Chama na TAKUKURU.
Kila
mwana-CCM wa dhati awe askari wa mstari wa mbele katika mapambano dhidi
ya adui rushwa kama ilivyo imani ya mwana CCM.
UCHAGUZI BILA RUSHWA UNAWEZEKANA, KILA MWANACHAMA, TIMIZA WAJIBU WAKO.!
Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
15/05/2012
No comments:
Post a Comment