Mwigulu Nchemba
Kabwe Zitto
Nimesikitishwa na kushangazwa na
taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari hivi na Mbunge wa
Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Zuberi Kabwe.Mimi nilikuwa ni Mchumi Daraja la Kwanza katika Benki Kuu ya Tanzania na nilikuwa nafanya kazi kwenye Kurugenzi ya Utafiti wa Uchumi na Sera.
Hivyo, nafahamu jinsi Benki Kuu
inavyofanya kazi. Na nasikitika kwamba wanasiasa sasa, katika
kujitafutia umaarufu, tunaingia kwenye kushambulia taasisi muhimu
inayoendeshwa kwa weledi na uadilifu mkubwa.
Baada ya Mhe. Zitto Kabwe kukosa taarifa muhimu mtandaoni, ningetegemea Mbunge kama Zitto, ambaye Kamati yake inakagua mahesabu ya BOT, kuwasiliana na Benki na kuuliza kulikoni, badala ya kusambaza taarifa katika vyombo vya habari kulaani Benki Kuu na kusambaza tetesi kuhusu hali ya Hazina ya Taifa.
Lakini vilevile, ningetegemea kwamba,
kama ameamua kusambaza taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, basi
taarifa hiyo ingejumuisha yale aliyoyabaini baada ya kuzungumza na Benki
Kuu.
Yeye kama kiongozi, kama anaamua kuwasiliana na umma kwa kusambaza
taarifa kwa vyombo vya habari, basi walau aonyeshe umma jitihada
nyingine alizofanya za kupata ripoti hizo zaidi ya kwenda tu mtandaoni,
kwasababu sote tunajua kwamba hata namba ya Gavana wa Benki Kuu anayo.
Pili, kutokuwepo kwa ripoti mtandaoni hakumaanishi kwamba ripoti hizo aidha zimefichwa au hazipo. Ni muhimu sana viongozi wakawa wa kweli na wakaacha mtindo wa kungoja siku ambayo haina habari (Jumapili) na kuamua kutengeneza habari kwa ajili ya vichwa vya habari vya Jumatatu.
Naomba kutoa ufafanuzi wa jinsi
ukweli ulivyo, kwasababu hata sisi katika Chama tumekuwa tunafuatilia
taarifa hizi za Uchumi kutoka Benki Kuu.
Kwanza, katika taarifa yake Zitto anaomba taarifa za mwezi Januari, Februari, Machi na Aprili zitolewe.
Hili limenishangaza kwasababu nilitegemea kwamba mtu kama Zitto, ambaye ni mchumi na ambaye kamati yake hupitia hesabu za BOT, angefahamu kwamba ripoti ya mwezi husika inaanza kuandaliwa tarehe 15 ya mwezi unaofuatia – kwa maana kwamba report ya mwezi Machi ilianza kuandaliwa tarehe 15 Aprili, report ya mwezi Aprili, itaanza kuandaliwa tarehe 15 Mei, na report ya mwezi Mei itaanza kuandaliwa tarehe 15 Juni.
Huu ni
utaratibu wa kimataifa, ambapo inategemewa kwamba katika kipindi hicho
cha wiki mbili baada ya mwezi kuisha, takwimu muhimu kutoka sehemu
mbalimbali zitakuwa zimekusanywa na kuhakikiwa.
Pili, ningetegemea pia Mhe. Zitto awe anafahamu kwamba kabla ya taarifa hizi za Benki Kuu kuchapishwa ni lazima zipitishwe na Kamati ya Sera za Fedha ya Bodi ya Benki Kuu (Monetary Policy Committee of the Board).
Huko nyuma, Kamati
hii ilikuwa inakutana kila mwezi, lakini kutokana na maagizo ya Kamati
ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mhe. Zitto kwamba vikao katika
Benki Kuu vipunguzwe. Hivyo, ikaamuliwa kwamba Kamati hii inayopitisha
taarifa hizi muhimu iwe inakaa mara moja kila baada ya miezi miwili.
Matokeo yake ni kuchelewa kupitia na kupitisha taarifa hizi muhimu. Mara
ya mwisho kikao kilikaa mwezi Machi kupitia taarifa ya mwezi Januari,
ambayo imekwishasambazwa.
Tatu, si kweli kwamba Hazina ya Fedha za Kigeni Taifa imekauka. Ambacho angeweza kufanya Zitto na ana mamlaka hayo na uwezo anao ni kumpigia simu Gavana au wasaidizi wake na kuwauliza ni kiasi gani cha Hazina kilichopo.
Mimi ndicho nilichofanya,
na taarifa rasmi, ni kwamba hazina iliyopo ni kiasi cha dola za
kimarekani bilioni 3.6, ambazo zinawezesha kuagiza mahitaji yetu yote ya
bidhaa kwa kipindi cha miezi minne, na wala sio mwezi mmoja kama
alivyodai Mhe ZITTO.
Na akiba ya watanzania iliyoko kwenye
benki zetu nchini ni takribani dola za kimarekani 1.8 bilioni na
taarifa hii pia IMF wanayo, (taarifa hii ni kwa kipindi kinachoishia
tarehe 11 May 2012).
Binafsi nimesikitika sana kwamba kiongozi anaweza
kuwa irresponsible kiasi hiki cha kusambaza taarifa za uvumi wakati anao
uwezo wa kupata taarifa sahihi za maandishi na kuujulisha umma ukweli.
Mwisho, napenda kumsihi Mbunge mwenzangu kwamba ni muhimu kuwa makini na kutokurupuka katika mambo muhimu kama haya na ni muhimu kufanya utafiti kidogo kabla ya kuwasiliana na umma kwani sisi viongozi tunasikilizwa na kuaminiwa na watu na tunategemewa kuwa sahihi na wakweli wakati wote.
Imetolewa na:
Mwigulu Lameck Nchemba (MB)
Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa
Dodoma
13 Mei 2012
No comments:
Post a Comment