WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amewakaanga viongozi wenzake wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuweka bayana kuwa wamezidiwa nguvu na rushwa.
Sitta amewataka wananchi kutofanya makosa kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kutowachagua viongozi wasioweza kupambana na rushwa ambayo imechangia umaskini wa Watanzania na kuyumbisha uchumi wa nchi.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akitoa hotuba kwenye Tamasha la waandishi wa habari lililofanyika Msasani Club jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kwa sasa nchi inajitahidi kuwa na mwelekeo mpya.
Alisema mwelekeo huo mpya utaondoa ulaji rushwa wa wazi wazi bila kificho uliosababisha kusuasua kwa maendeleo yaliyokusudiwa.
Alisema rushwa ni adui wa haki, ndiyo maana kukithiri kwake kumeziathiri sekta nyingi na kudumaza maendeleo ya Tanzania ambayo ina rasilimali nyingi.
Sitta alisema kutokana na viongozi wa nchi hii kukumbatia rushwa kumesababisha waingie mikataba ya kitapeli na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi ambayo imewaumiza zaidi wananchi.
Sitta pia aliwataka viongozi wa kada mbalimbali kwenye vyama vya siasa, serikali na asasi mbalimbali kukubali kukosolewa pindi wanapoona wamekosea badala ya kujenga chuki na wale wanaowakosoa.
Alisema wapo wanasiasa wasiopenda kukosolewa na wamekuwa wakitoa vitisho kwa waandishi wa habari wanaofichua maovu yao.
Alisema vyombo vya habari ni kioo cha jamii, hivyo vina wajibu wa kukosoa makosa yoyote ya yule anayekiuka maadili ya uongozi.
“Vyombo vya habari ni rafiki kwa kiongozi yeyote yule muadilifu na haviogopi lakini ni mwiba mkali kwa yule ambaye anakwenda kinyume cha miiko ya uongozi.”
Alisema yeye ni rafiki wa vyombo vya habari na amekuwa akipokea changamoto nyingi zinazotolewa na vyombo hivyo katika uongozi wake.
Aliongeza kuwa anaamini vyombo hivyo vina wajibu wa kumkosoa ili aweze kutenda kazi zake za kila siku kiuadilifu.
“Nawashangaa viongozi wa serikali wanaoviona vyombo vya habari kama adui wao pale vinapokosoa utendaji kazi wao na kufichua uovu wao, au wanavyotumia vibaya madaraka yao kinyume cha dhamana walizopewa,” alisema.
Sitta amewataka viongozi kuviona vyombo vya habari kuwa msaada wa muhimu katika utendaji wao wa kazi.
“Kiongozi makini na mkweli anayesimamia masilahi ya nchi hawezi kuviogopa na kuanzisha vita kati yake na vyombo vya habari, nawaomba waandishi wa habari msiogope wala kutishwa na watu au viongozi wanaotaka maovu yao yasifichuliwe,” alisema.
Sitta pia aliwataka waandishi wa habari kutokubali kubebeshwa habari za uongo au kutumiwa kwa ajili ya masilahi ya watu fulani wasio na malengo mema kwa taifa.
Alisema kama waandishi wa habari wakikataa kutumiwa watajijengea heshima katika jamii, pia wataifanya tasnia yao izidi kushamiri na kuwa kioo cha kuonyesha maovu na mema.
“Kama uongo ungekuwa unauzwa, basi nchi hii ingetajirika sana, kwakuwa watu wengi kila kukicha wamekuwa wakitunga na kuzungumza uongo,” alisema.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment