Wednesday, March 28, 2012

Mahabusu waliotoroka kituo cha Polisi wakamatwa


Kituo kikuu cha Polisi Mkoa wa Mbeya


Mahabusu mwingine wa mauaji aliyetoroka katika Kituo kiku cha Polisi jijini Mbeya akiwa na wenzake watatu amekamatwa akiwa mafichoni wilayani Mbozi.


Maneno Wiwa Kalinga na wenzake walitoroka wiki iliyopita, amekamatwa saa 10 alfajiri katika kijiji cha Ruanda wilayani humo.


Kamanda wa Polisi mkoani hapa Advocate Nyombi, amethibitisha kukamatwa kwa mahabusu huyo na kufanya jumla ya waliokamatwa kufikia wawili.


Mwenzake Fadhili Mwaitebele (27) mkazi wa Ilomba jijini Mbeya alikamatwa muda mfupi baada ya kutoroka usiku wa kuamkia Machi 22.


Mahabusu wanne wakiwemo washitakiwa watatu wa mauaji walivunja mahabusu ya kituo cha kati (Central) Mbeya na kutoroka.


Kamanda Nyombi alisema, mahabusu hao walitoroka usiku wa manane kati ya saa nane na saa tisa.


Alisema, mmoja kati ya mahabusu waliotoroka , Mwaiteleke anakabiliwa na shitaka la wizi wa betri tatu za gari.


Alisema, mahabusu hao waliokuwa katika moja ya vyumba vipya vilivyoongezwa katika upanuzi na uboreshaji wa mahabusu ya kituo cha kati uliofanyika hivi karibuni walifungulia maji na kulainisha ukuta kwa kuumwagia maji kabla hawajatumia vipande viwili vya nondo kuchimba ukuta huo na kutoroka.


Alisema askari waliokuwa zamu ya usiku katika chumba cha mapokezi ya mashitaka kama kawaida yao ya kukagua mahabusu kila baada ya saa moja walifika katika chumba hicho na kusikia maji yakimwagika kwa wingi hali iliyoonesha bomba lilikuwa limeachwa wazi.


Baada ya kuchunguza walibaini kuwa mahabusu wanne waliokuwamo walikuwa wametoroka kupitia tundu lililochimbwa ukutani na kukuta vipande viwili vya nondo vilivyoachwa vinavyosadikiwa kuwa kuna mtu aliyeviingiza humo kutoka upande wa nje kupitia matundu madogo yaliyopo upande wa juu wa ukuta


Kamanda huyo amefafanua kuwa baada ya askari hao kubaini kutoroka kwa mahabusu walitoa taarifa kwa vyombo vingine vya usalama na kwa ushirikiano wa pamoja usiku huo wakafanikiwa mahabusu Mwaiteleka akiwa katika jitihada za kutokomea mbali zaidi.


Picha na habari kwa hisani ya blog ya Mbeya Yetu.

No comments:

Post a Comment