Friday, January 27, 2012

Wagonjwa Muhimbili waambiwa warudi nyumbani

Wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam wameambiwa warudi nyumbani hadi watakapopata taarifa za kumalizika kwa mgomo kupitia vyombo vya habari.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wagonjwa hao wamesema, walipewa taarifa na baadhi ya wafanya kazi katika vitengo tofauti, vinavyotoa huduma za kliniki hospitalini hapo.


Vitengo vilivyodaiwa kuwatangazia habari hiyo wagonjwa hao ni Taasisi ya Mifupa (MOI), kitengo cha kuhudumia watoto wenye matatizo ya upungufu wa damu na kitengo cha Kliniki ya matatizo ya moyo.


Mmoja wa wagonjwa hao, Rukia Hamisi alisema alipofika MOI alitokea mmoja wa wafanya kazi katika taasisi hiyo na kuwatangazia kuwa wagonjwa wote waondoke eneo hilo hadi watakapotangaziwa kuwa mgomo umekwisha.


“Mimi nimekuja tangu asubuhi, lakini ilipofika saa tatu asubuhi alikuja mfanyakazi mmoja na kututangazia kuwa tuondoke katika eneo hilo hadi tutakapo tangaziwa kuwa mgomo umekwisha kupitia vyombo vya habari,” alisema Hamisi.


Mmoja wa wafanya kazi wa MOI ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, alikiri kutoa taarifa hizo na kusisitiza kuwa hali hiyo imetokana na madaktari wanaotakiwa kuwahudumia wagonjwa hawakuwapo kazini.


Muhonewa Mfaume ambaye alikwenda hosptalini kwa ajili ya kutaka barua yake aliyopewa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iweze kusainiwa na daktari ili aweze kwenda kutibiwa nje ya nchi, alisema alipofika katika kitengo hicho aliambiwa na mmoja wa wafanyakazi wa idara ya mapokezi kwamba, arudi nyumbani


Afisa Habari Mwandamizi wa Hosptali ya Taifa Muhimbili Aminiel Aligaesha alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alijibu kwa kifupi kuwa hana taarifa na pia akasisitiza kuwa, huduma zinazoendelea vizuri.


KCMC nako mambo yaharibika Mgomo huo umezidi kutikisa nchi na kuvuruga huduma za utabibu baada ya madaktari katika hospitali ya Rufaa ya KCMC ya mjini Moshi nao kujiunga rasmi kwenye mgomo.


Hata hivyo, madaktari hao wamekubaliana kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura tu wakiwamo wa ajali, wanaohitaji kujifungua na walioko wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu(ICU).


Katika tamko lao hilo, madaktari hao waliokutana katika ukumbi wa maktaba walisema katika kipindi chote cha mgomo hawatapokea wagonjwa wa nje na kwamba kliniki zote hazitafanya kazi.


Ingawa hospitali hiyo inamilikiwa na Shirika la Msamaria mwema (GSF) lakini wapo madaktari ambao mikataba yao ya ajira ipo chini ya shirika hilo na wapo ambao ajira zao ziko moja kwa moja serikalini.BugandoJana madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando waliungana na wenzao katika mgomo unaoendelea kusambaa nchi nzima hivi sasa.


Madaktari hao walianza mgomo kwa kukataa kuwapokea wagonjwa wapya isipokuwa wagonjwa wa dharura tu.Wakizungumza wakati wa mkutano wao uliofanyika katika hosteli ya madaktari wanafunzi, walisema kurudi kwao kazini kutategemea maelekezo kutoka kwa uongozi wa kamati maalum waliyoiunda kuratibu mgomo huo.


Juhudi za uongozi wa hospitali hiyo chini ya Mkurugenzi wake, Dk Charles Majinge kuzuia mgomo huo ziligonga mwamba baada ya madaktari hao kumweleza kuwa mgomo huo haujaitishwa dhidi ya hospitali hiyo wala uongozi wake na kwamba, madai yao yako nje ya uwezo wa utawala wa Bugando.


Dk Majinge alikataa kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mgomo wa madaktari katika hospitali yake.BundaHuduma ya tiba kwenye baadhi ya vituo vya afya wilayani Bunda, jana zilidorora kufuatia baadhi ya madaktari na wahudumu kuitisha mgomo.


Mwananchi imebaini kuwa ingawa wahudumu na madaktari hao wamefika kazini kwa wakati lakini walikataa kuwahudumia wagonjwa.


“Mimi nimefika hapa saa 3:00 asubuhi lakini sijahudumiwa. Wanaingia (wahudumu) wanakaa ndani kisha wanatoka bila kuwaita wagonjwa," alisema mmoja hospitalini hapo saa 8:00 mchana jana.


Kaimu mganga mkuu wa wilaya hiyo Dk Fransic Mayengera alikana uwepo wa mgomo hospitalini hapo na huku aiita hatua hiyo kuwa ni kutokana na uzembe wa watumishi wa hospitali na kwamba uongozi wake umeanza kuwashughulikia."


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment