Jana jioni katika mizunguko ya hapa na pale nilifika katika pub maarufu Kinondoni iitwayo Matema, nikaagiza kinywaji, mhudumu akasema nimpe fedha.
Haikuwa kawaida, nikampigia simu Hassan maarufu kwa jina la Hasanoo kwa sababu ndiye niliyemzowea na kila ninapokwenda hapo huwa ananihudumia yeye kwa bili.
Nilidhani alikuwa ndani kwa sababu sikumuona pale counter au miongoni mwa wahudumu waliokuwa pale nje.
Alipokea mwanamke, nikaomba kuongea na Hassan, nikaambiwa Hassan hatunaye duniani!
Sikumwelewa, nikamuuliza tena, akanijibu kwamba 'Hassan amefariki na sasa tupo njiani tunakwenda Tanga kumzika'.
Nilimwambia 'hembu acha utani, naomba kuongea na Hassan'
Alinijibu kwamba, yeye ni mke wa Hassan, na kama siamini, niende Kinondoni B, kuna baa inaitwa Matema, nikamuulize dada (jina nimelisahau).
Nikamwambia nipo hapo Matema ndiyo maana nimempigia Hassan.
Nilikata simu na sikuzingaita kauli kwamba Hassan amefariki, nilidhani ulikuwa utani!
Sekunde kadhaa baada ya hapo alikuja mhudumu mwingine wa hapo Matema ambaye anafahamu kwamba mimi na Hassan ni marafiki, alikuwa ameshika picha na daftari.
Baada ya salamu akaniambia rafiki yako Hassan amefariki dunia, dah.
Nilikumbuka kauli ya mkewe na nilichoambia hapo Matema, kumbe kweli rafiki yangu Hasanoo kaaga dunia.
Nilimfahamu Hassan tangu akiwa muhudumu Twiga Pub iliyopo Namanga, Dar es Salaam, tukawa marafiki, na hata alipohamia Matema urafiki wetu uliendelea.
Wakati anafanya kazi Twiga, mkewe alikuwa anafanya biashara ndogondogo jirani na hapo, walikuwa na mtoto mmoja wa kike.
Nimeambiwa kwamba hivi sasa ni mjamzito anakaribia kujifungua.
Hassan kaaga dunia juzi (Jumanne) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Aligongwa na pikipiki wiki moja iliyopita wakati anavuka Kinondoni B, aliumia kichwani.
Jana usiku niliongea na mjane akanieleza kuwa walikuwa safarini kwenda Tanga nyumbani kwa akina Hassan kwenda kumzika.
Buriani rafiki yangu Hasanoo, nakumbuka namna ulivyonihudumia mara ya mwisho pale Matema, aksante kwa upendo wako kwangu.
Nasikitika kwa sababu sikupata taarifa kuwa ulipata ajali, ningekuja kukuona hospitali na pengine kuna kitu ungeniambia.
Nenda Hasanoo umemaliza safari yako, kapumzike, umetangulia.
No comments:
Post a Comment