Friday, December 9, 2011

Posho mpya za wabunge- Ni Makinda Vs Kashililah

SAKATA la nyongeza ya posho za wabunge sasa limegeuka vita baina ya watendaji wakuu wa taasisi hiyo ya kutunga sheria; Spika Anne Makinda na Katibu wake, Dk Thomas Kashililah.


Hali hiyo inaonekana baada ya Dk Kashililah jana kuendelea kusisitiza kuwa kauli yake kwamba posho hizo hazijaanza kutolewa kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete hajasaini, bado ni sahihi na kuahidi kuweka mambo hadharani akirejea nchini kutoka jijini London.


Dk Kashililah alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili akiwa London Uingereza kuhusu mgongano wa kauli na msimamo kuhusu posho hizo, uliojitokeza baina yake na Spika Makinda.


“Mimi ni Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Bunge. Na ninapozungumzia jambo nina uhakika na kile ninachokizungumza kwa kuwa najua wajibu wangu,”alisema Dk Kashililah.


Alisisitiza kuwa kauli aliyoitoa awali, inatokana na kile alichokuwa akikifahamu kwa mujibu wa mamlaka yake ya kiutendaji na madaraka aliyonayo kwenye ofisi hiyo ya Bunge.


Dk Kashililah alisema hana wasiwasi na kauli yake na hivyo akaomba apewe muda kwa kuwa wakati mwingine siyo vyema kuzungumzia jambo linalohusu ofisi akiwa nje ya nchi.


“Njoo ofisini (Jumatatu) nikisharudi nitalielezea vizuri jambo hilo,” alisema alipotakiwa na gazeti hili kuelezea juu ya misimamo iliyotolewa na baadhi ya viongozi wa dini, wasomi, wanaharakati na wanasiasa kumtaka ajiuzulu kutokana na kauli yake kuonekana kuwa ya uongo hasa baada ya Makinda kueleza kuwa posho hizo zimeshaanza kulipwa.


Dk Kashililah alisema anafahamu vyema wajibu wa mamlaka aliyonayo hivyo ataweka wazi ukweli wa mambo siku hiyo atakapoingia ofisini.


Alifafanua kwamba anatarajia kurejea nchini wakati wowote mwishoni mwa wiki hii na Jumatatu atakuwa ofisini kwake Dodoma, tayari kutoa ufafanuzi huo.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment