Thursday, December 15, 2011

Mume adaiwa kukodi watu wamuue mkewe

POLISI wilayani Nkasi mkoani Rukwa inamshikilia raia wa Burundi anayedaiwa kukodiwa kumuua kwa kumkata kiuno na shoka mwanamke aliyetambuliwa kuwa ni raia kutoka Zambia ili mume wa marehemu aweze kurithi kirahisi mali za mwanamke huyo ambaye anadaiwa kuwa ni 'tajiri sana.'


Inadaiwa mtuhumiwa akiwa na wenzake wawili ambao wanatafutwa na Polisi wakiwa na mashoka, walimvamia mwanamke huyo na kukata kiuno chake kwa shoka kiasi cha kutenganisha mwili wake sehemu mbili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage kwanza amemtaja mshtakiwa kuwa ni Abdul Selemani (30) mkazi wa mjini Kumonge, Burundi.


Kamanda Mantage alimtaja marehemu huyo kwamba ametambuliwa kuwa ni Beauty Muntali (39) ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa eneo la Mpata mjini Mpulungu, nchi jirani ya Zambia.


Akihadithia mkasa huo wa kusikitisha, Mantage alidai kuwa mama huyo alifikwa na mauti hayo juzi, saa mbili usiku katika kijiji cha uvuvi cha Kampumpuli kilichopo mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi.


Inadaiwa kuwa mwanamke huyo akiwa amefuatana na mumewe, Noal Muyaya waliwasili katika kijiji hicho cha Kampulimpuli wakitokea Mpata –Mpulungu.


“Wanandoa hao walifika kijijini Kampumpuli kwa ajili ya shughuli zao za biashara ya kununua samaki na dagaa,” alisema Mantage.


Inadaiwa wanandoa hao walipofika Kampulimpuli walifikia nyumbani kwa mwenyeji wao, Lucas Tuseko ambapo usiku mwanamke huyo akiwa amepumzika na mumewe, alifika msichana, Jane Mpimbwe na kumwita.


Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, msichana huyo alimtaka marehemu aende ziwani kuchukua dagaa kwa ajili ya kitoweo.


Inadaiwa aliongozana na msichana huyo hadi ziwani ambapo muda mfupi baadaye zilisikika taarifa kuwa Beauty amejeruhiwa vibaya na shoka kiunoni ambapo alifariki dunia papo hapo.


Mantage alidai uchunguzi wa awali ulibaini kuwa ameuawa na watu waliotumwa na mumewe ili amiliki mali za marehemu kwani inadaiwa mama huyo alikuwa na mali nyingi kwao Zambia.


“Katika jitihada za kuwasaka waliotenda kosa hilo, ndipo Polisi walipofanikiwa kumkamata raia wa Burundi Abdul ......alipohojiwa alikiri kufanya mauaji hayo akishirikiana na wenzake wawili wote raia wa Burundi,” alibainisha Mantage.


Kwa mujibu wa Kamanda Mantage, mtuhumiwa huyo aliungama kwa kueleza kuwa kabla ya kutenda ukatili huo, mume wa mwanamke huyo aliwapeleka kwa mganga wa kienyeji ambapo walipigwa chale mwili mzima na kunyweshwa dawa ili wafanikishe mauaji hao na wasikamatwe wala kushukiwa na Polisi.


Kamanda Mantage alisema mume wa marehemu amekamatwa ambapo juhudi za kupata watuhumiwa waliotoroka akiwemo mganga wa kienyeji zinaendelea.


Chanzo: Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment