Thursday, December 22, 2011

Maafa Dar es Salaam

WATU 11 wakiwamo watatu wa familia moja, wameripotiwa kufa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia mvua zilizoendelea kunyesha jana katika Jiji la Dar es Salaam na viunga vyake na kuvuruga mfumo wa usafiri na shughuli za kiuchumi.


Miondombinu mbalimbali ya Jiji hilo ikiwamo madaraja na nyumba vilivunjwa na kusababisha adha kubwa kwa wakazi ambao wengi wao, walishindwa hata kwenda kazini.


Baadhi ya barabara zikiwamo Morogoro eneo la Jangwani na Ali Hassan Mwinyi eneo la daraja la Salenda zilifungwa kwa muda kutokana na kujaa maji kiasi cha kuhatarisha maisha ya watumiaji wake.


Mvua hiyo ya siku mbili mfululizo kunyesha jijini Dar es Salaam, jana ilifanya maeneo mengi zikiwamo barabara muhimu kama Nyerere kuanzia Uwanja wa Ndege, Kawawa eneo la Kigogo Darajani na Mandela eneo la Tabata Matumbi, kushindwa kupitika kwa saa kadhaa kutokana na kujaa maji.


Katika barabara ya Mandela hali ilikuwa tete baada ya maelfu ya abiria waliokuwa wanasafiri kutoka Buguruni kwenda Ubungo, kukwama katika daraja la Matumbi.


Kwa zaidi ya saa nne tangu saa 1:00 asubuhi abiria walioonekana wakishuka kutoka kwenye magari na kutembea kwa miguu mithili ya maandamano, huku makumi ya magari yakiwa yamezimika barabarani.


Wakati hayo yakitokea, watumiaji wa barabara ya Mandela walikwama kutokana na msururu mrefu wa magari kufuatia baadhi yake kuzima na kufunga barabarani.


Katika barabara hiyo eneo la TIOT, ulionekana moshi mkubwa angani uliotokana na moshi wa gesi baada ya bomba linalopitisha gesi hiyo kupasuka.


Moshi huo uliwafanya watu waliokuwa kwenye magari kupatwa na vikohozi.


Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetaja mvua zilizonyesha jana na juzi kuwa hazijawahi kutokea katika miaka ya karibuni, na kwamba mara ya mwisho mvua kubwa kama hiyo ilirekodiwa mwaka 1954.


Baadhi ya madaraja yalisombwa au kuvunjwa na maji hivyo kusababisha shida ya usafiri katika jiji hilo.Daraja la Mbezi katika barabara ya Morogoro lililoko jirani na kibanda cha mkaa eneo la Tanesco lilivunika na kusababisha kukatika mawasiliano ya safari za kutoka na kwenda katikati ya jiji.


Mawasiliano katika daraja hilo yalikatika saa 11:00 alfajiri, na kusababisha misururu ya magari yaliyokuwa yakisubiri maji yapungue ili yapite.


"Hii leo sio kawaida, heri ya jana, sisi tumekwama tangu saa 10:30 alfajiri na mpaka sasa 1:45 asubuhi hatujui tutaondoka saa ngapi," alisema mmoja wa abiria waliokwama eneo hilo, ambaye alipiga simu ofisi za gazeti hili bila kutaja jina lake.


Vitus Andrew aliyejitambulisha kuwa ni dereva wa gari aina ya Mitsubishi fuso, alisema alifika eneo hilo saa 11.20 alfajiri na kukuta msururu wa magari ukiwa hautembei hivyo kumalazimu kuzima gari na kulala.


“Ndugu yangu, nimefika hapa mapema nikiwa naelekea Tabora, lakini naona safari yangu imeishia hapa kwa leo na kibaya zaidi hakuna kiongozi ama askari yeyote aliyefika kusimamia usalama wa abiria na magari kwani hali ya usalama si nzuri,” alisema Andrew.


Taarifa zilizopatikana baadaye, zilisema magari yalianza kupita kwenye daraja hilo saa 2:20 asubuhi.Daraja la Mbezi Bondeni linalounganisha Mbezi Beach na Mwenge, wilayani Kinondoni limekatika upande mmoja kutokana na mafuriko hivyo kufanya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha Lugalo kuweka kambi maalumu kwa ajili ya kulinda usalama.


Hatua hiyo imesababisha wananchi wanaotoka Mbezi kuelekea Mwenge, kushindwa kutumia magari na kulazimika kuvuka kwa miguu kutokana na magari yote kuzuiwa kupita eneo hilo.


Daraja lililopo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilijaa maji hivyo kulazimisha uongozi wa jeshi kuzuia magari yasipite kwa muda.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment