Friday, December 23, 2011

Kikwete- Mnaoishi mabondeni hameni

RAIS Jakaya Kikwete amewahakikishia waathirika wa mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku tatu mfululizo sasa, kuwa Serikali itawapa msaada wa hali na mali, lakini lazima wahame mabondeni.


Amesema Serikali ipo tayari kuwatafutia maeneo ya kujenga makazi ya kudumu na kwa dharura iliyopo kuwapa hifadhi ya mahema, vyakula, magodoro, vyoo, maji na huduma ya afya kama ilivyofanyika, lakini haina msamaha juu ya wao kuendelea kuishi mabondeni.


“Wenzetu wa hali ya hewa wanasema mvua hizi zinaendelea, Makamba (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kabla ya Abbas Kandoro) aliwahamisha kwa helikopta, sasa Sadiki (Said Mecky-Mkuu wa Mkoa wa sasa) naye anawahamisha vivyo hivyo, hivi hali hii tutaiacha ijirudie mpaka lini?.....


“Ni vizuri mjiondoe kwenye maisha ya mashaka, nawahakikishia Serikali yenu ipo nanyi katika hali ngumu hii, lakini ni vizuri muondoke maeneo hayo ya hatari, suala kubwa ni mnahamaje? Kamati ya Maafa ya Mkoa ihakikishe hilo linatekelezwa kwa ubora na mapema,” alisema Kikwete akizungumza na waathirika hao.


Alizungumza na waathirika walio katika Kambi ya Mchikichini, wilayani Ilala, wapatao 1,900 kwa niaba ya waathirika wengine wa kambi nyingine saba zilizowekwa katika shule za sekondari na msingi kwa hifadhi.


Kabla ya kuzungumza nao, Rais Kikwete alipata nafasi ya kuzunguka kwa helikopta kuona athari za mafuriko hayo katika jiji na pia kutembelea kambi hiyo.


Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, watu zaidi ya 20 wamepoteza maisha na 4,900 wameathirika kwa kukosa makazi. Aidha, vifo zaidi havijaripotiwa kwa kuwa bado baadhi ya nyumba zimezingirwa na maji na matope.


Akihutubia hadhara hiyo, Rais alisisitiza watu kuheshimu mikondo ya maji kwa kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kuzuia maji, upepo au moto na kutolea mfano kwa Marekani, Australia na nchi zenye teknolojia ya juu, lakini maji huwashinda.


Rais Kikwete aliwaagiza Mipango Miji wafanye kazi ipasavyo kwa kuwa wao ndio wamekuwa vinara wa kugawa maeneo kwa hati halali wakati wakijua wazi ni maeneo hatari kwa maisha ya watu, mabondeni na kwenye mikondo ya maji.


“Maji hayana tajiri wala masikini, nilikuwa napita kwa helikopta nikaona hata kwenye kampuni ile Jangwani (Kajima) ukuta umeenda, Mipango Miji fanyeni kazi vizuri kuepusha yanayoweza kuepukika, mikondo ya maji iachwe nafasi, baadhi ya hawa watu wana hati halali, mmewapa ninyi,” alisema Rais.


Aidha, aliwahakikishia waathirika hao kufuatiliwa kwa karibu suala lao na kuwaahidi kuwa viongozi wakiwemo mameya, wabunge, madiwani na watendaji wahakikishe usiku na mchana watawahudumia mpate makazi maeneo yafaayo.


wali, akihutubia, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki alisema walioathirika ni 4,900 na vifo vilivyoripotiwa mpaka jana asubuhi ni 20 ambapo miili 18 imetambuliwa na miwili bado ipo Hospitali ya Taifa Muhimbili, aliwataka watu wakatambue miili hiyo.


Katika hotuba yake, Sadiki alisema uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na viongozi wa kisiasa wamefikia hitimisho la kuwataka wakazi hao wa mabondeni kuridhia kuhama baada ya kutenga eneo katika Wilaya ya Kinondoni la ekari 2,000 linalotoa viwanja 2,800 ili wakazi hao waanze kujenga makazi mapya.


“Lakini tuna taarifa huko nyuma kwamba kuna waliopewa maeneo Wazo Hill, Yombo Dovya, hawakuhamia huko, wakauza na hata hizi huku wakauza, muda si mrefu shule zitafunguliwa hivyo tutahakikisha mnapata hifadhi ya dharura huko ili tuwapishe wanafunzi huku,” alisema Sadiki.


Kwa mujibu wake, kuna kambi zaidi ya saba jijini Dar es Salaam na vitu mbalimbali vimetolewa na wasamaria wema, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi yakiwemo mahema, vyakula, nguo, dawa na mikeka.


Mbunge wa Ubungo, John Mnyika ametoa vitu vyenye thamani ya Sh milioni moja kwa kambi tano. Gazeti hili lilitembelea katika baadhi ya kambi hizo kwa lengo kujionea hali ilivyo ambapo katika kituo cha Rutihinda, hadi saa 5.45 asubuhi, waathirika 52 waliokuwa wameandikishwa walilalamika kutokuwepo kwa huduma yoyote ikiwemo ya chakula, na magodoro tangu wafike kambini hapo juzi asubuhi.


Akizungumzia suala hilo, msimamizi wa kambi hiyo ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Kigogo, Kassim Mbezi, alisema iliwalazimu baadhi ya waathirika kuondoka na kujitafutia hifadhi na chakula. Walikuwa zaidi ya 100 kambini hapo na kubaki hao 52.


“Hadi hivi sasa watu waliopo hapa ni 52, awali waliokuwepo wengi lakini wanapokuja na kukuta hali ya kambi ilivyo wanaamua kuondoka na kurudi katika maeneo waliyotoka na wengine kwenda kujitafutia chakula kwa kuwa wana watoto,” alisema Mbezi.


Chanzo: Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment