Monday, December 5, 2011

Buriani Alfred Ngotezi

MWANDISHI wa habari mkongwe nchini, Alfred Ngotezi (56), amefariki dunia juzi usiku mjini Arusha ambako alikwenda kikazi.


Mdogo wa marehemu, Jamhuri Ngotezi alithibitisha kifo cha kaka yake na kueleza mipango ya mazishi inaendelea na kwamba atazikwa kijijini kwao katika Jimbo la Buchosa wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza.


Jamhuri alisema mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Dar es Salaam leo. Ngotezi alifariki dunia akiwa katika hoteli moja jijini Arusha ambako alikuwa akipata chakula cha usiku pamoja na marafiki zake Jumamosi usiku.


Mashuhuda wanaeleza kwamba alianguka wakati akienda msalani, wakati mwingine wanaeleza kuwa alianguka wakati akirejea katika meza yake baada ya kutoka kucheza muziki uliokuwa ukiporomoshwa hotelini hapo.


Taarifa kutoka Arusha zinaeleza kuwa Ngotezi aliyekuwa Ofisa Habari Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Jamii (NSSF) mjini Dar es Salaam, alikuwa mwenye hali ya furaha na afya njema wakati akiwa na wafanyakazi wenzake kwa chakula cha usiku katika Hoteli ya Rombo View, Mianzini jijini Arusha.


Ngotezi aliyezaliwa Desemba 11, 1955, alisoma katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Bwiru jijini Mwanza, kabla ya kujiunga na Sekondari ya Mzumbe Morogoro.


Baadaye, alisomea Materials Management katika Taasisi ya Maendeleo Mzumbe (IDM), kabla ya kuonesha mapenzi katika uandishi wa habari.


Alisomea Shahada ya Uzamili katika Uandishi wa Habari katika Chuo cha Cardiff nchini Uingereza, kabla ya kurejea nyumbani na kujikita katika fani hiyo, akiwa mwandishi mahiri. Hadi mauti yanamkuta, alikuwa akisimamia masuala ya Elimu kwa Umma katika Idara ya Uhusiano ya NSSF.


Alikuwa pia Mhariri wa jarida la shirika hilo, Hifadhi. Aidha, alikuwa akiandika safu iliyobeba jina la ‘Thinking Aloud’ katika gazeti la Sunday News, ambalo ni miongoni mwa magazeti ya Tanzania Standard Newspapers (TSN) Limited. Mengine ni Daily News, HabariLeo na HabariLeo Jumapili.


Ngotezi alikuwa Arusha pamoja na maofisa wengine wa NSSF wakiandaa mkutano wa Mifuko ya Jamii kwa Ukanda wa Afrika, ukiratibiwa na Chama cha Kimataifa cha Mifuko ya Jamii (ISSA) kwa ushirikiano na NSSF.


Mkutano huo wa siku tatu unaanza leo. Ndugu, jamaa na marafiki wanakutana nyumbani kwa marehemu, Tabata Kisiwani jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi ya Ngotezi ambaye ameacha mjane Modesta, na watoto sita, Ivon, Batuli, Philomena, Veronica, Bernard na Faustine.


Chanzo: Gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment