Wednesday, December 7, 2011

Alfred Ngotezi kuzikwa leo Sengerema

MWANDISHI mkongwe nchini, Alfred Ngotezi (56) aliyefariki dunia ghafla Jumamosi akiwa Arusha kikazi, anatarajiwa kuzikwa leo kijijini kwao Nyakarilo, Kata ya Nyakarilo, wilayani Sengerema mkoani Mwanza.


Safari ya kuelekea Mwanza kutokea nyumbani kwake Tabata Kisiwani, Dar es Salaam, ilianza juzi jioni baada ya misa katika Kigango cha Mtakatifu Padri Pio.


Kabla ya misa, juzi nyumbani kwa marehemu ibada fupi ilifanyika na kisha mamia ya waombolezaji pamoja na familia yake walipata fursa ya kuuaga mwili wa mpendwa kwa kutoa heshima za mwisho.


Mdogo wa marehemu, Jamhuri Ngotezi akiwa safarini jana, alisema walifika Mwanza salama na jana alasiri walikuwa katika kivuko cha Busisi wakivuka kwenda Sengerema kijijini Nyakarilo tayari kwa maziko leo.


“Hatuwezi kusema kwa usahihi ratiba ikoje kwa kuwa bado tupo safarini, lakini kwa machache tulionayo ni kwamba tunatarajia kuzika kesho (leo) kuanzia saa tisa alasiri Mungu akitujalia,” alisema Jamhuri.


Ngotezi alifariki ghafla akiwa Arusha kikazi na taarifa zinaeleza kuwa kifo chake kimetokana na shinikizo la damu, tatizo hilo lilithibitishwa pia na mkewe Modesta aliyedai kuwa mumewe alikuwa na tatizo hilo, lakini wakati akiondoka nyumbani Dar es Salaam kuelekea Arusha, alikuwa mzima wa afya.


Mbali na kuwa Ofisa Habari Mwandamizi wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Jamii (NSSF), Ngotezi alikuwa akiandika safu iliyobeba jina la ‘Thinking Aloud’ katika gazeti la Sunday News la Tanzania Standard Newspapers (TSN) Limited. Mengine ni Daily News, HabariLeo na HabariLeo Jumapili.


Alizaliwa Desemba 11, 1955 na kusoma Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Bwiru, Mwanza kabla ya kujiunga na Sekondari ya Mzumbe, Morogoro, baadaye alisomea Materials Management katika iliyokuwa Taasisi ya Maendeleo Mzumbe (IDM) kabla ya kuonesha mapenzi katika fani ya habari.


Alisoma Shahada ya Uzamili katika Uandishi wa Habari katika Chuo cha Cardiff nchini Uingereza kabla ya kurejea nchini na kujikita katika uandishi na kuwa mahiri.


Ngotezi ameacha mke na watoto watano wakiwemo watatu wa kike.


Chanzo: gazeti la HABARILEO

No comments:

Post a Comment