MADAKTARI wa Hospitali ya Apollo iliyopo Bangalore, India kesho (Jumatano) watamfanyia upasuaji Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto.
Zitto alipelekwa India kwa matibabu zaidi ya maradhi ya kipanda uso ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa miaka 10 sasa.
Akizungumza na Mwandishi wa gazeti la The Citizen akiwa India, Zitto alisema afya yake imeimarika na kwamba maradhi ya kipanda uso yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda sasa yamepungua.
“Afya yangu imeimarika sana kwa sasa.. ninasubiria upasuaji. Madaktari wamenieleza kwamba watanifanyia upasuaji huo kesho kutwa Jumatano (kesho),” alisema.
Naibu kiongozi huyo wa kambi ya upinzani bungeni alisafirishwa kwenda India akisumbuliwa na maradhi ya malaria, yaliyokuwa yakitibiwa MNH ambako alifikishwa baada ya kushindikana kwenye Hospitali ya Aga Khan.
Katika taarifa yake ndefu aliyoituma kwenye ukurasa wa Facebook mwishoni mwa wiki, Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema alisema alikuwa akisumbuliwa na maradhi hayo kwa takribani miaka 10 sasa.
Alisema kuwa kwa nyakati kadhaa alikuwa akipoteza fahamu na madaktari wa Muhimbili walipompima walipendekeza afanyiwe upasuaji kama njia nzuri ya kuweza kuyaondoa maradhi hayo.
Zitto aliondoka Ijumaa iliyopita kwenda India akimbatana na kaka yake, Salum Kabwe na mmoja wa wauguzi wa Muhimbili ambaye jina lake halikufahamika mara moja.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment