Tuesday, November 22, 2011

Mwendesha bodaboda awanyang'anya majambazi bastola

MWENDESHA pikipiki zinazofanya biashara ya kubeba abiria maarufu ‘bodaboda’ amewapora bastola majambazi wawili wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.


Hata hivyo majambazi hao, walimpora kijana huyo pikipiki aliyokuwa akiitumia.


Mwendesha pikipiki huyo aliyejitambulisha kw ajina la Athuman Juma, alikabiliana na majambazi hao katika eneo la klabu ya Biashara, Temeke.


Purukushani hiyo ilianza mara tu kijana huyo alipoanza kudai malipo yake kwa mteja aliyemsafirisha kutoka kituo chake cha Vetenary, Temeke.


Akizungumza katika ofisi za Mwananchi, Juma alisema,juzi saa moja usiku mtu huyo alifika katika kituo hicho cha Vetenary na kumtaka ampeleke katika ukumbi huo wa klabu ya Biashara, Temeke.


Amesema, baada ya kumfikisha eneo la klabu hiyo, alipokuwa akidai malipo yake alijitokeza mtu mwingine kutoka ndani ya ukumbi huo aliyekuwa na bastola na kumuamuru kushuka kwenye pikipiki, akitaka pia amkabidhi simu yake ya kiganjani.


Juma alisema, baada ya kuona hivyo, aliamua kushuka kwenye pikipiki na kumkabidhi mteja huyo aliyekuwa amemkodi lakini akafanikiwa kumshika kijana huyo aliyekuwa na Bastola, ndipo walipoanza kupambana wakiing’ang’ania bastola na kusababisha risasi moja kufyatuka bila kumdhuru yeyote miongoni mwao.


Alisema baada ya purukushani hizo alifanikiwa kumnyang`anya jambazi huyo bastola, na baada ya kuona wamezidiwa nguvu waliamua kukimbia na pikipiki wakitokomea kusikojulikana.


“Vurugu ilikuwa kubwa ya kunyang`anyana ile bastola, lakini niliwashinda na kuweza kuchukua bastola, ndipo wakakimbia na pikipiki maana walikuwa wameshachukua funguo,” alisema.


Alisema baada ya tukio hilo kutokea alijitokeza mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa yeye ni askari wa upelelezi jijini Dar es Salaam na kumtaka kupeleka bastola hiyo kituo cha Polisi cha Kilwa Road ili aweze kuandika maelezo.


“Hakika wakati wa tukio lile niliogopa sana kutokana na wale watu kuwa na bastola lakini baada ya kupata ujasiri nilipambana nao na kuwashinda,” alisema.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi wa kuwatafuta majambazi hao na kuwasihi wananchi kuwapa polisi ushirikiano wa kutosha.


Misime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la ujambazi na kushukuru kijana huyo kwa ushujaa alioonyesha wa kupambana na majambazi hao na kusihi kuwa Jeshi la Polisi litatoa zawadi kwa wananchi wanaoshirikiana na jeshi hilo katika kuimarisha ulinzi shirikishi.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment