Tuesday, November 8, 2011

Mnyika kuufufua mjadala wa Richmond

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), amesema amewasilisha taarifa ya nia katika Ofisi za Bunge, ili awasilishe hoja binafsi bungeni akitaka mjadala wa kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond ufufuliwe upya ili wabunge wajadili maazimio yote 23 ambayo hayakufanyiwa kazi.


Akizungumza na gazeti hili jana mjini hapa, Mnyika alisema taarifa ya hoja aliiwasilisha Ijumaa iliyopita na hadi sasa hajapata majibu ya lini awasilishe hoja hiyo bungeni katika mkutano unaoanza leo.


“Kifungu cha 55 cha kanuni za Bunge kinaruhusu siku moja kabla ya Bunge kuanza, Mbunge anaweza kuwasilisha hoja binafsi… sasa ni mwaka mmoja tangu mjadala ufungwe wakisema Serikali ingefanyia kazi maazimio 23, haijafanya kitu na wahusika hawajafungwa wako mtaani. Nataka wabunge wajadili ili wachukuliwe hatua,” alisema Mnyika.


Alisema taarifa ya hoja ameiwasilisha kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2007 Kanuni 54 (4) na 55 (1).


Awali, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mnyika alisema “Lengo la Hoja Binafsi nitakayoiwasilisha kufuatia taarifa hii ni kutaka uamuzi wa Bunge uliofanyika katika Bunge la Tisa Mkutano wa 18 Februari 2010 kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya mkataba baina ya Tanesco na kampuni ya Richmond Development Company LLC; ubadilishwe,” alisema.


Aliendelea: “Katika muktadha huo, hoja hii itawezesha mjadala kuhusu uamuzi husika kufunguliwa na kutoa fursa kwa jambo hilo kufikiriwa tena, ili kuwezesha hatua kamili kuchukuliwa juu ya maazimio 23 ya Bunge yaliyopitishwa tarehe 15 Februari 2008 katika Mkutano wa 10 wa Bunge la Tisa.”


Iwapo ataruhusiwa, ataiwasilisha katika Mkutano wa Tano wa Bunge la 10 unaoanza leo kwa kadri itakavyoelekezwa.Aidha, katika mkutano huo, Muswada wa Sheria wa Mapitio ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, ukitarajiwa kutikisa Bunge wakati utakapowasilishwa na kujadiliwa na wabunge.


Sambamba na hilo, katika mkutano huo, Kamati Teule ya kuchunguza sakata la kusimamishwa na kurejeshwa kazini kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, inayoongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani, itawasilisha taarifa yake na kujadiliwa na wabunge.

Endapo Muswada huo utapitishwa kuwa sheria, Rais ataunda Tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba na kuunda Bunge la Katiba kwa madhumuni ya kutunga Katiba mpya.


Kwa mujibu wa Muswada huo, Rais atateua wajumbe wa Tume hiyo itakayokusanya maoni ambao ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na makamishna wasiozidi 30. Uteuzi huo utazingatia usawa wa pande mbili za Muungano.


Muswada huo unabainisha kuwa wanasiasa wakiwamo wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, madiwani, watumishi wa vyombo ya usalama au watuhumiwa ambao shauri lake liko mahakamani la kukosa uaminifu au maadili, hawatateuliwa katika Tume hiyo.


Bunge la Katiba litaundwa na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, mawaziri wenye dhamana ya Katiba ya Serikali ya Muungano na Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano na Zanzibar.


Pia wamo wajumbe 116 watakaoteuliwa kutoka asasi zisizokuwa za Serikali, asasi za kidini, vyama vya siasa vilivyo na usajili wa kudumu, taasisi za elimu ya juu na makundi yenye mahitaji maalumu.


Sheria hiyo itaruhusu kupigwa kura ya maoni ambapo wananchi watapiga kura ya kutaka au kutotaka Katiba mpya na Tume ya Uchaguzi ya Taifa na ya Zanzibar ndizo zitakazosimamia.


Tayari asasi za kiraia na baadhi ya vyama vya siasa ikiwamo Chadema, wameupinga Muswada huo wakisema Rais amepewa mamlaka makubwa na uliharakishwa bila kushirikisha wananchi wengi kutoa maoni yao.


Taarifa iliyotolewa na Bunge kupitia Idara yake ya Habari, Elimu kwa Umma na Mahusiano ya Kimataifa mwishoni mwa wiki, ilisema Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa ili kuchunguza uhalali wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa taasisi zake ili kupitisha bajeti ya wizara hiyo, itawasilisha taarifa ya uchunguzi.


Taarifa hiyo itabainisha endapo kitendo cha Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo cha kutoa taarifa kwa wanahabari juu ya uchunguzi wa suala la fedha zilizochangishwa kiliingilia na kuathiri madaraka ya Bunge.

Mkutano huo wa Bunge utaanza kwa kuapishwa wabunge wapya, Dk. Dalaly Kafumu wa Igunga (CCM) aliyechaguliwa katika uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni na Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Mohammed Said Mohammed aliyeteuliwa kujaza nafasi ya marehemu Mussa Amme Silima, aliyefariki dunia wakati wa Mkutano wa Bunge la Bajeti.


Shughuli nyingine zitakazofanywa na Mkutano huo wa Bunge, ni kujadili miswada mitatu ya sheria za Serikali ukiwamo huo wa Marekebisho ya Katiba.


Miswada mingine ni pamoja na wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali za Biashara wa mwaka 2011 na wa Sheria ya Manunuzi ya Umma wa mwaka 2011.


Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi (Chadema) atawasilisha hoja binafsi kuhusu madhara ya uwekezaji kwenye sekta ya ardhi na madhara yake kwa wananchi.


Hata hivyo, hoja hiyo itawasilishwa kwanza ili kuona kama inakidhi kanuni ya 54 ya Kanuni za Kudumu ya Bunge toleo la mwaka 2007.


Kutafanyika pia semina kwa wabunge kuhusu matumizi ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la 2007, semina kuhusu muswada wa Sheria ya Mapitio ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011 na warsha kwa wabunge kuhusu Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.


Katika Mkutano huo wa Bunge, jumla ya maswali 125 yanatarajiwa kuulizwa katika vikao vyote tisa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ataulizwa maswali ya papo hapo yapatayo 16.

No comments:

Post a Comment