MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amebainisha tatizo linalomsibu akisema madaktari wamemweleza kwamba anasumbuliwa na ugonjwa wa kipanda uso unaofahamika kitalaamu kama sinusitis ambao kwa hatua uliokuwa umefikia, tiba yake isingepatikana nchini.
Kutokana na kubainika kwa maradhi hayo, amesema anatarajia kufanyiwa upasuaji wakati wowote kuanzia sasa huko India anakotibiwa.
Zitto alieleza hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, katika ulingo wa wazi wa majadiliano ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika wenye zaidi ya wanachama 3,110.
“Tatizo lililogundulika ni sinusitis, ambayo tayari imekuwa sugu. Daktari Bingwa wa magonjwa haya, Dk Kimaryo (wa Muhimbili) akanieleza kwa kirefu juu ya tatizo hili na kuniambia suluhisho ni 'surgery' (upasuaji) na pale Hospitali ya Taifa hawafanyi hiyo operesheni,” alisema Zitto.
Naibu Kiongozi huyo wa upinzani Bungeni, alisema kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo Dk Kimaryo alishauri apelekwe India ambako kuna daktari bingwa mpasuaji wa ugonjwa huo...
“Baada ya kuwa malaria imedhibitiwa kwa kufikia nusu ya dozi niliyopewa na wadudu kuonekana kutokomea, Ofisi ya Bunge ikaandaa safari. Nimefika India. Nimebakiza sindano mbili ili kumaliza dozi hiyo na tayari nimefanyiwa taratibu zote kwa ajili ya 'surgery' hiyo.”
Juzi, Zitto alipelekwa India baada ya kufanyiwa uchunguzi wa maradhi yanayomsumbua katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako alibainika kuwa na vijidudu 150 vinavyosababisha ugonjwa wa malaria.Sunusitis ni ugonjwa gani?
Akizungumzia ugonjwa huo, Dk Idd Mujungu wa Hospitali ya Wilaya ya Ulanga alisema ni ugonjwa unaofahamika na wengi kama kipanda uso.
“Kwenye kichwa cha mwanadamu kuna matundu ya hewa ambayo kitaalamu yanaitwa simus. Kipanda uso kinaweza kuyaziba matundu hayo kama ni cha siku nyingi na ikifikia hatua hiyo, upasuaji ni lazima.”
Alisema dalili nyingine za kipanda uso ni mgonjwa kutokwa machozi, kichwa kuumwa sana, macho kuwa mekundu na kuwa na mafua makali.
Zitto alisema tatizo hilo lilimuanza takriban miaka 10 iliyopita na katika kipindi chote hicho, amepoteza fahamu na kuanguka mara nne.
“Mara ya kwanza mwaka 2000 nikiwa Mwanza nikielekea kwenye Mkutano wa Vijana wa National Youth Forum, mara ya pili Dodoma katika mkutano kama huo mwaka 2001, lakini ilikuwa usiku.
Mara ya tatu nilikuwa chumbani Hall II, mara baada ya kutoka ‘prep’ (kujisomea), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2002 na mara ya Nne Bungeni siku ya kupitisha Muswada wa Madini 2010 kufuatia wiki nzima ya Kamati na Mjadala wa Bunge," alisema na kuongeza:
“Nilianza kupatwa na maumivu ya kichwa usiku wa Ijumaa tarehe 20, (Oktoba, mwaka huu) Dar es Salaam mara baada ya kuwasili kutoka jimboni tayari kwa kazi za Kamati za Bunge ambapo Kamati yangu ilikuwa imekwishaanza kazi wiki hiyo kwa kupitia mahesabu na utendaji wa mamlaka za maji nchini.”
“Kama kawaida yangu niliona maumivu hayo makali kama ni sehemu tu ya uchovu wa ziara za jimboni na safari za mara kwa mara nilizofanya ikiwamo kuhudhuria Mdahalo wa Umeme na Mkutano wa Uwekezaji Kanda ya Ziwa Tanganyika.
Hivyo nililala na nilipoamka kichwa kilikuwa kimepona na hivyo nikahudhuria kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma katika Ofisi ya Bunge mpaka saa saba mchana.”“Siku ya Jumapili saa 11:00 jioni nikiwa katika Hoteli ya Southernsun nilipatwa na homa kali ghafla.
Nilikatisha mkutano niliokuwa nao na kuamua kurejea nyumbani, lakini nilishindwa kuendesha gari na hivyo kumwomba dereva wa mheshimiwa Mhonga (Saidi Ruhwanya Mbunge wa Viti Maalumu Chadema), anifuate ili anisaidie kunifikisha nyumbani.”
“Nilipofika nyumbani kwangu Tabata, homa ilizidi kupanda na hivyo kuamua kwenda Hospitali mara moja. Nikapelekwa Aga Khan Hospital na nikapata huduma. Walituliza homa, nikapewa Panadol na baadaye nikaruhusiwa kurudi nyumbani mnamo saa tano usiku. Nilipoamka siku ya Jumatatu nikaenda kazini kuongoza Kikao cha Kamati ya Bunge ambapo tulikuwa tunashughulikia hesabu za Bodi ya Utalii na Benki ya Posta Tanzania.”
“Nilipita Aga Khan kupata majibu ya ziada na kuambiwa nipo sawa ila nipumzike nisifanye kazi kwa siku kadhaa na nitakuwa sawa.”
“Siku ya Jumanne, niliamka nikiwa salama, kichwa kikiuma kwa mbali lakini siyo vya kutisha. Nikawajulisha wajumbe wenzangu wa kamati kuwa sitakwenda kazini na wao waendelee na kazi. Ilipofika saa 6:00 nilianza kutetemeka mwili mzima na homa kuwa kali sana huku kichwa kikiniuma sana sana sana!”
Alisema alipelekwa tena Hospitali ya Aga Khan na vipimo kubainisha kuwa alikuwa na joto la nyuzi 39.8 na kupatiwa matibabu.Alisema usiku wa Jumatano hali ilikuwa mbaya na joto lilipanda tena kufikia nyuzi 40 na kichwa kilianza kuuma zaidi na kuongeza...
“Nilikuwa kama ninatwangwa kwenye kinu kwa kweli. Nilikuwa natetemeka sana. Ilikuwa taharuki kubwa sana katika chumba nilicholazwa.
”Alisema wageni waliofika kumjulia hali wakati hali inabadilika walikuwa Murtaza Mangungu na Mohamad Chombo ambao ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC)...
“Walishauri mara moja nihamishiwe Muhimbili.”
“Muda si mrefu kupita Waziri Lukuvi (William, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge) na Katibu wa Bunge walifika, wakaafiki na nikahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kwa hali niliyokuwa nayo nikalazwa katika chumba wanachokiita mini-ICU.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Blandina Nyoni alikuwapo hospitalini tayari,” alisema.Alisema usiku huo alifanyiwa vipimo upya...
“Ikaonekana nina wadudu wa malaria 150 na mara moja nikaanza matibabu. Namshukuru sana daktari kijana Dk Juma Mfinanga kwa umahiri mkubwa aliouonyesha tangu nilipofika pale mini ICU.”
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment