WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda, leo amelieleza Bunge kuwa, hakuvunja Katiba kwa kuamua kumsubiri Rais Jakaya Kikwete arudi nchini kumchukulia hatua Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo.
Jairo aliandika barua ya kukusanya Sh. milioni 50 kutoka kila idara za wizara hiyo ili ziwezeshe kupitishwa kwa bajeti ya wizara hiyo.
Pinda amewaeleza wabunge kuwa, ni kweli kuwa wakati tuhuma hizo zinazoashiria wabunge kuhongwa zilipotolewa bungeni Rais hakuwepo, Makamu wa Rais, alikuwepo, lakini unapokaimu urais huwezi kufanya uamuzi kadri unavyojisikia.
Waziri Mkuu amesema, unapokaimu urais unakuwa na mipaka ya kufanya uamuzi, na kwamba, maana ya kukaimu madaraka hayo ni kurahisisha mawasiliano na mkuu wa nchi katika utekelezaji wa majukumu ya kuiongoza serikali.
Pinda alisema jana kuwa, alimjulisha Rais Kikwete mambo yaliyotokea Jumatatu bungeni kuhusu mjadala wa Makadirio na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini ambapo baadhi ya wabunge walitaka Jairo aondolewe.
“Amenijibu kuwa ‘sawa, nisubiri nitakaporudi Afrika Kusini tuone tunafanyaje’,” alisema Pinda nje ya ukumbi wa Bunge akimnukuu Rais Kikwete.
Jumatatu wakati wa mjadala wa makadirio hayo, wabunge waliibua kashfa wakituhumu wizara hiyo kuchangisha Sh bilioni moja kutoka idara na taasisi zake kwa ajili ya kufanikisha uwasilishaji wa makadirio hayo.
Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), aliibua sakata hilo wakati akichangia hotuba ya Makadirio hayo kabla hayajaondolewa bungeni.
Shelukindo aliwasilisha barua bungeni iliyoandikwa na Jairo ikizitaka idara na taasisi zote za wizara hiyo, kila moja ichangie Sh milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya uwasilishaji wa hotuba ya bajeti.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), na Shelukindo, kwa nyakati tofauti, walihoji bungeni mantiki ya fedha hizo, takribani Sh bilioni moja na wakataka wizara ifafanue zimekusanywa kwa ajili gani.
Pinda alikiri kwamba Jairo aliudhi na kutibua wabunge ana aliahidi kumjulisha Rais Kikwete ili achukue hatua.
“Lazima nikiri hata mimi nilishtuka sana tena si kidogo, kwani suala hili limegubikwa na maswali mengi hakuna namna ya kutetea,” alisema.
Duuh, mkuu tumeinyaka hiyo shukurani TUPO PAMOJA
ReplyDelete