Wednesday, July 13, 2011

Bunge lachafuka tena

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amewaponda wabunge kutoka Kambi ya Upinzani katika Bunge la Tanzania kwa kusema kuwa ni wanafiki hivyo wabunge wa CCM wawavumilie.


Sitta alitoa kauli hiyo alipokuwa akituliza Bunge lililochafuka baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), kudai kuwa Serikali ni legelege.

"Nawasihi wenzangu hasa wa CCM, hawa wapinzani hii (kupinga mambo) ndiyo kazi yao, wanabeza kila tunachofanya kwa lugha nyepesi nyepesi na mambo mengi wanayozungumza ni unafikinafiki hivi, sisi tuwaachie wananchi wawahukumu"

Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge hasa wa upande wa upinzani kusimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, na wengine wakizomeana.


Maneno ya wabunge yaliyokuwa yanasikika ni kama vile: "…cha ubishi…", "…so what…," "…hiyo siyo taarafa…," "…hujui…" "Nani hana heshima nani, hana heshima…"


Kwa sasa Sitta ni Kaimu Kiongozi wa Shughuli za
Serikali Bungeni.

"Subirini nitoe mfano ... wanazungumza posho za vikaoni ni kuibia
wananchi na baadhi yao wamekuwa wabunge kwa miaka mitano
iliyopita na walikuwa wakizichukua, kama kweli ndivyo hivyo, basi warudishe," alisema Sitta.


Kabla ya kuibuka tafrani hiyo, Kafulila aliyekuwa akichangia hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, alisema tangu Uhuru moja ya maadui waliopigwa vita ni maradhi; lakini akashangaa bajeti ya Afya ni ndogo na kuongeza kuwa inatokana na Serikali legelege kushindwa kukusanya mapato.

"Miaka 50 ya Uhuru asilimia 90 ya bajeti ya maendeleo ya afya inategemea fedha za nje, tatizo hamkusanyi kodi na Nyerere (Baba wa Taifa) alisema Serikali legelege inashindwa kukusanya kodi," alisema Kafulila.

Kauli hiyo ilipingwa na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangala (CCM) aliyesema Kafulila alitumia neno la kuudhi kwa kuiita Serikali ya CCM legelege.

Dk. Kigwangala alifafanua kuwa Kafulila hakuwa na taarifa sahihi, kwa kuwa katika miaka mitatu iliyopita, Serikali ilikuwa ikikusanya karibu Sh bilioni 200, lakini mpaka mwaka huu, makusanyo yaliongezeka na kufikia karibu Sh bilioni 400.

Baada ya kuona hivyo Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama alisema: "Hata kama mnazungumza huko, kauli ninayoitoa mimi ndiyo yenye nguvu, kwa kuwa ni Spika wa kikao hiki."


Pamoja na Mhagama kusisitiza kuwa anaposimama kuzungumza, au mtu mwingine anapopewa ruhusa na Spika, au Mwenyekiti kuzungumza, mtu mwingine hairuhusiwi kuwasha kinasa sauti na kuzungumza, wabunge hawakuvizima na wakaendelea kuzungumza bila utaratibu.


Mhagama alimtaka Kafulila kufuta usemi, lakini Mbunge huyo alipinga akisema ni kauli ya Baba wa Taifa, ambaye kila mtu anamuenzi bila kujali anatoka chama gani.

"Tunapoteza muda kujadili suala ambalo liko wazi, mwaka 2005/06 Serikali ilikuwa ikikusanya wastani wa Sh bilioni 260 lakini dola moja ilikuwa sawa na Sh 1,000.

"Leo mnakusanya karibu Sh bilioni 400 kwa mwezi, dola moja ni Sh 1,600 ni hesabu rahisi, hakuna kilichoongezeka ... sifuti usemi, niko tayari kufia ukweli huu," alisema Kafulila.

Hata hivyo, Mwalimu Nyerere alisema chama legelege huzaa Serikali legelege na pia aliwahi kusema "Serikali corrupt (inayokula rushwa) hushindwa kukusanya kodi," na si Serikali legelege hushindwa kukusanya kodi.

Awali, kabla ya tafrani hiyo, Kafulila alimtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, ajiuzulu kuliko kukubali kuwasilisha bajeti ya fedha ndogo bungeni.

Alisema hiyo inatokana na wabunge na familia zao kuwa na uwezo wa kutibiwa sehemu yoyote ndani na nje ya nchi, ndiyo maana hawawekezi katika hospitali za vijijini.

Wakati akisema hayo, mmoja wa wabunge ambaye hakufahamika lakini mwanamke, aliwasha kipaza sauti akasema: "Pamoja na wewe (Kafulila) na Mbunge wa Mpanda Mjini Chadema (Said Arfi ambaye alilazwa India hivi karibuni)."

Hata hivyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, alisimama na kupinga kauli ya Kafulila, akisema: "Hili ni Bunge Tukufu, tuzungumze kwa heshima."

Mbunge mwingine mwanamume akawasha kipaza sauti na kuhoji: "Nani ana heshima?"

Nagu aliwaeleza wabunge kuwa, mwanawe ni daktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambayo ni ya Serikali na hata baba yake mzazi alilazwa katika hospitali ya Katesh ambayo ni ya vijijini.

Hata hivyo, sauti ile ya kiume iliendelea kumkatisha Nagu na safari hii Mbunge huyo alisema, "so what (kwa hiyo?)"

No comments:

Post a Comment