Thursday, July 28, 2011

Bunge lachafuka tena, Mbunge atimuliwa

Harakati za kumtoa nje Wenje
Wenje anaeleza alitaka kuzungumzia nini kwenye jambo hilo la dharura

Ilikuwa dharau, zogo, kuzomeana na kutoheshimu kanuni za Bunge, sasa ni dhahiri kwamba hadhi ya Mhimili huo wa Dola inazidi kushuka kwa kuwa sasa wabunge wanasutana!


Wabunge kutoka Kambi ya upinzani jana walimsuta Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe baada ya Mbunge huyo kumweleza Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje kuwa alikosa ustaarabu kwa kutomtii Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba.


Mabumba alimuamuru Wenje atoke nje ya ukumbi wa Bunge baada ya Mbunge huyo kusimama na kutaka kuzungumza jambo alilosema ni la dharura bila ruksa ya Mwenyekiti wa Kikao.


Wenje hakutii amri ya Mwenyekiti wa Bunge, ikatolewa amri kuwa atolewe kwa nguvu, wahusika wakatekeleza wajibu wao.


Baada ya Filikunjombe kusema Wenje hakuwa mstaarabu, wabunge walimvaa, wakashutumu na kumsuta kuwa alikosa uzalendo kwa kuwa mwenzake alitaka kuzungumzia jambo la msingi linalogusa afya za wananchi.


Kwa mujibu wa Wenje, Kanuni za Bunge zinamruhusu Mbunge kuzungumzia jambo la dharura, na kwamba, yeye alitaka kuomba Bunge lijadili suala la samaki wanaodaiwa kuwa na sumu walioingizwa nchini kutoka nchini Japan.


Kulikuwa na zogo kubwa nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma, wabunge walimzonga Filikunjombe na nusura wampige.
Filikunjombe (wa pili kushoto) ilibidi awe mpole.

Wenje (wa tano kushoto mwenye suti nyeupe) aliungana na wenzake kumshushia Filikunjombe mzigo wa lawama.


Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu


Picha zote kwa hisani ya blog ya Prince-Minja

No comments:

Post a Comment