Wednesday, July 13, 2011

Breaking News- Rostam ajivua gamba,aponda siasa ndani ya CCM

Mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Aziz amejiuzulu ubunge na nafasi zote za uongozi alizokuwanazo katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Rostam alikuwa pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiuwakilisha Mkoa wa Tabora.


Rostam ametangaza uamuzi huo leo Igunga mkoani Tabora, na kubainisha kwamba, amefanya hivyo kuepuka siasa uchwara, vita vya ovyo ndani ya chama hicho na kwa faida ya biashara zake.


Amesema, yeye ni mfanyabiashara wa kimataifa hivyo ni muda muafaka kwake kuachia ngazi na haoni sababu ya kuendelea kuvutana na viongozi wa CCM.

Amewaeleza wazee wa Igunga kwamba, hajajiuzulu kwa sababu ya shinikizo la kujivua gamba ila anaepuka siasa uchwara ndani ya CCM, na anafahamu kuna watu watapotosha mantiki ya uamuzi wake.


Rostam amesema, hana muda wa siasa uchwara zilizomo CCM, anakaa kando aendelee na biashara zake na maisha yake.


Blog hii ina hotuba yote ya Rostam, ifuatayo ni sehemu ya hotuba hiyo.


Wazee wangu, nimetafakari sana na kimsingi nimefikia hatua ya kupima yale ambayo yamekuwa yakisemwa na kuandikwa juu yangu na ambayo kwa mtazamo wangu unaoungwa mkono na wanafamilia yangu, marafiki zangu na washirika wangu wa kibiashara walio ndani na nje ya nchi, naona umefika wakati muafaka wa kuchukua hatua.


Kwa sababu ya kutambua uzito wa hatua ninazokusudia kuzichukua, niliona halitakuwa jambo la hekima hata kidogo iwapo ningefanya hivyo pahala pengine popote bali hapa Igunga mbele ya nyie wazee wangu.


Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.


Wazee wangu, sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara.


Athari kama hizo za kibiashara huingia ndani zaidi kuliko vichwa vya habari vya magazeti vinavyolenga kuchafuana, na athari hizo huwa kubwa zaidi kwa mtu kama mimi kwa sababu tofauti na wengine wengi hapa nchini, mimi ni mfanyabiashara wa kimataifa.


Katika ulimwengu wa kibiashara wa leo, vita hivi ambavyo vinaweza kuonekana kuwa ni vidogo tu vyenye malengo ya kuchafuana kisiasa, vinakuwa na athari kubwa katika uhusiano wa kibiashara kuliko hata wale wasioelewa wanavyoweza kukadiria.


Ndiyo maana nimeona ni afadhali sasa niwape nafasi wale wanaoendesha siasa hizi uchwara na zisizo na tija waendelee na siasa zao hizo ambazo kwa bahati mbaya kwao, mimi sina muda nazo na siwezi kuwa sehemu yake. Na mimi kwa upande wangu niendelee na maisha yangu.


Kutokana na ukweli huo na sababu zote hizo basi, kwa moyo wa dhati na kwa nia thabiti, hatua ya kwanza niliyoiona kuwa ninapaswa kuichukua ilikuwa ni hii ya kuitikia wito unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi yangu wa kuamua kukomesha kabisa malumbano na mivutano isiyo na manufaa kwangu binafsi, kwa viongozi wa chama changu na chama chenyewe.


Msukumo huo si mwingine bali ni ule wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu nisingelikuwa nazo.


Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu.


Aidha, nimefikia uamuzi huo lengo likiwa ni kuwajengea heshima na imani machoni mwa wanachama na wananchi wengine, viongozi wangu ambao naamini baada ya mimi kujitoa watapata fursa ya kutafakari upya changamoto nyingine mbadala zinazowakabili ambazo msingi wake ni dhamana kubwa walizo nazo za kukiongoza chama chetu na nchi yetu kupitia Serikali yake.


Wakati nachukua uamuzi huu, natambua vyema kwamba, watatokea watu ndani ya chama chetu na nje ambao watafanya kila juhudi kupotosha au kupindisha ukweli kuhusu hatima yangu ya kisiasa baada ya kujiweka kando na kujipa mimi mwenyewe na chama changu fursa ya kutafakari kwa kina majaaliwa yangu na ya nchi yangu katika siku zijazo.


Nafanya hivyo nikiwa na imani thabiti kwamba, uamuzi wangu huu, hususani ule wa kuachia nafasi yangu ya ubunge, yatakipa fursa nyingine CCM ya kuendelea kuliongoza jimbo letu la Igunga katika kipindi cha miaka minne ijayo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.


Kwa upande mwingine, uamuzi wangu huu naona ni fursa kwa viongozi wa Chama changu cha CCM kutafakari na kuamua njia wanayoiona wao ni sahihi kuichukua kwa hatima na mustakabali wa chama chetu na ambayo wanaamini itakipa nguvu mpya ya kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani.


Sambamba na hilo, ninayo imani thabiti kwamba, uamuzi wangu wa kubakia kuwa mwanachama wa kawaida na mtiifu wa CCM utakuwa chachu kwa chama changu na kwa Serikali yake kuwatumikia wananchi kwa Ari Zaidi, Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi.

No comments:

Post a Comment