Saturday, June 25, 2011

Kusoma kuelewa, kukesha mbwembwe tu

Bila shaka upo ‘poa’, na ‘mishemishe si za kitoto’ wakati huu tunapoendelea kupambana na changamoto za kila siku, wape ‘hi’ wadau, tupo pamoja.


Namshukuru Mungu sijambo, mambo si mabaya, ‘laifu’ linabana lakini hatoki mtu, tutabanana hapa hapa hadi kieleweke, kama wao walishindana na wakashinda kwa nini nisiweze?


Ujumbe wangu kwako leo ni kwamba, unaweza kuwa ‘kilaza’ darasani lakini ukawa fundi mzuri wa nguo, umeme, magari, mbao, au ukafanya biashara hadi watu wakashangaa, ili utoke si lazima uwe na diploma au shahada, na si wote wenye elimu hiyo wametoka.


Itumie hiyo elimu uliyonayo kujitambua halafu ufanye uamuzi wa ama, kwenda kidato cha tano, kusoma chuo cha ufundi au cha taaluma nyingine au kufanya mambo mengine ya maendeleo unayoyaweza.


Umri ulionao ni muhimu sana katika kufanya uamuzi wa busara kuhusu mwelekeo wa maisha yako, ni wakati wa kuwa na msimamo, kukataa shinikizo la kufanya hata yale usiyoyapenda, na kuamua kwa kutambua kwamba kuna kesho ya kwako, amua wewe kwa faida yako, hatma ya maisha yako ipo kwako.


Usilazimishe kufanya usiyoyaweza, nilipomaliza kidato cha nne nilikuwa na upeo wa kujitambua, nilifahamu kwamba siwezi kuwa daktari, rubani au mhasibu, na niliamua kusomea kile nilichokiweza ili nifanye kazi ninayoipenda.


Mimi naamini kwamba kila mtu ana kipaji fulani, ni bahati mbaya kwamba wengi hawavitambui vipaji vyao na hawaoni kwamba hilo ni tatizo.


Itumie siku ya leo kutambua kipaji chako na ujiulize kwa nini usikitumie kikutoe, na kama huwezi kukitambua, hao unaoishi nao, kukutana nao, au ‘kuchati’ nao wanaweza kukusaidia.


Jipe muda kujitambua ili ufanye uamuzi wa busara kwa ajili ya maisha yako, epuka kufuata mkumbo au kuiga, una utashi wa kuamua mema na mabaya, umepewa uhuru wa kufanya unachokiweza, lakini pia umepewa dhamana ya kutoyaharibu maisha yako ya kesho, kila la heri.

No comments:

Post a Comment