Monday, October 19, 2009

'Jisaidie kabla ya kupanda ndege'

SHIRIKA la ndege la Japan, All Nippon Airways (ANA) limeanzisha mbinu ya aina yake ya kubana matumizi na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Shirika hilo linawataka abiria wake waende chooni kwanza kabla ya kupanda ndege.

Shirika hilo lilisema kwamba abiria wakipanda ndege baada ya kujisaidia watakuwa wamepunguza uzito katika ndege na hivyo lita za mafuta ya ndege yatakayotumika zitapungua.

Shirika hilo la ndege linaweka wafanyakazi wake kwenye mageti ya njia zinazokwenda sehemu za kupanda ndege.

Jukumu la wafanyakazi hao ni kuwakumbusha abiria kwenda chooni kwanza kabla ya kupanda ndege.

Shirika hilo la ndege linaamini kwamba uzito utakaopungua kwenye ndege zao utasaidia kupunguza matumizi ya mafuta ya ndege na hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kiasi cha tani tano za gesi ya Carbon Dioxide katika kipindi cha mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa televisheni ya NHK ya Japan, shirika hilo la ndege lilianza majaribio ya mwezi mmoja ya mpango huo Oktoba mosi mwaka huu.

Kama majaribio hayo yataonyesha mafanikio kwa ndege zao 42 basi mbinu hiyo ya kubana matumizi itaendelezwa kwa ndege zote za shirika hilo.

No comments:

Post a Comment