Friday, October 9, 2009

Afya ya Rais Kikwete hadharani

DAKTARI wa Rais Jakaya Kikwete amesema kiongozi huyo hana matatizo yoyote ya kiafya.

Dk. Peter Mfisi, amesema, vipimo anavyofanyiwa kila mara Rais vinaonesha hana matatizo yoyote mwilini mwake zaidi ya maumivu ya shingo na wingi wa damu mwilini.

Ameyasema hayo wakati akizungumzia mjadala uliojitokeza kupitia vyombo vya habari hivi karibuni kuhusu afya ya Rais, baada ya kukatiza hotuba Jumapili iliyopita katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Wakati akizungumza uwanjani hapo,Rais Kikwete aliishiwa nguvu,na kwa mujibu wa daktari wake, tatizo ilikuwa ni uchovu wa safari.

Rais Kikwete alikwenda Kirumba kushiriki maadhimisho ya miaka 100 ya Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT).

“Wakati tukio hilo linatokea nilikuwapo, nilichukua vipimo muhimu kama daktari anavyotakiwa kufanya linapotokea tukio kama lile kwa mtu.

Vipimo vyote vilithibitisha kuwa Rais hakuwa na matatizo yoyote ya kiafya ambayo yangeweza kuhusishwa kuwa chanzo cha tukio lile,” alisema Dk. Mfisi.

Daktari huyo anasaidiana na daktari bingwa wa maradhi ya moyo katika Hospitali Kuu ya Taifa Muhimbili,Dk. Mohamed Janabi, kumtibu Rais Kikwete Dk Mfisi alisema, ingawa maadili ya kazi yake ya udaktari hayamruhusu kutoa siri ya ugonjwa wa mtu anayemtibu,kwa kuzingatia maslahi ya taifa na umma wa Watanzania, na kwa kuwa Rais mwenyewe ameridhia taarifa hizo zitolewe, aliamua kuzungumza na waandishi wa habari.

Akifafanua kuhusu vipimo alivyomfanyia uwanjani Kirumba muda mfupi baada ya kuzidiwa na uchovu, Dk. Mfisi alisema,msukumo wa damu yake ulikuwa wa kiwango cha 130/85mmhg ambacho ni cha kawaida kwa mtu wa umri wake.
Oktoba 7, Rais Kikwete alitimia umri wa miaka 59.

“Mapigo ya moyo wake yalikuwa 76 kwa dakika ambayo pia ni ya kawaida.
Sukari kwenye damu ilikuwa 5.5mmol/l ambayo nayo ilikuwa ya kiwango cha kawaida. Joto la mwili lilikuwa digrii 37.5 za sentigredi ambalo ni la kawaida.

Rais pia hakuwa na kiungo chochote kilichoonekana kutetereka, jambo ambalo lilithibitisha kuwa hakupata kiharusi,” alisema Mfisi na kuongeza ndiyo sababu akamruhusu kuendelea na sherehe.

Alisema,baada ya kurudi Dar es Salaam, aliwasiliana na madaktari wenzake wa ndani na nje ya nchi na kuwasimulia tukio na vipimo, walithibitisha kuwa tatizo lilikuwa ni uchovu kwa sababu wanaifahamu vizuri afya ya Rais Kikwete kwa kuwa mmoja wao alimchunguza siku moja kabla ya kuondoka New York, Marekani, kurejea nchini mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Napenda kuwahakikishia wananchi wenzangu kuwa katika miaka hii minne, Rais wetu amefanyiwa uchunguzi wa kina wa afya yake.
Nadiriki kusema kuwa hakuna kipimo ambacho hatujapata kukifanya katika uchunguzi wa mambo muhimu ya afya yake,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment