Friday, July 24, 2009

Wabunge washambuliana bungeni

Wabunge wawili leo wameshambuliana bungeni, mmoja kasema mwenzake anakera, mwingine kamtuhumu mwenzake kuwa ni muongo.
Wametuhumiana kwa nyakati tofauti wakati Bunge lilijadili bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka wa fedha 2009/10.

Mbunge wa Kasulu Magharibi, Kilontsi Mporogomyi, amesema, ndani ya Bunge kuna mambo yanakera na amewashutumu wabunge wanaozungumza bungeni bila kufanya utafiti kwanza.

Mporogomyi amesema wabunge wanapaswa kutoa hoja zenye mantiki ili wabunge wafaidike na si kutoa hoja zinazohusu ndugu zao.

Tuhuma alizotoa Mbunge wa Singida Kusini, Mohamed Missanga, jana zimemkera Mporogomyi na amesema kuwa, Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) linafanya kazi vizuri.
Mporogomyi amesema, ataipinga hoja binafsi ya Missanga ya kutaka iundwe tume huru ya Bunge kuichunguza NECTA.

Missanga jana alisema, Katibu wa Baraza hilo, Dk Joyce Ndalichako ni tatizo katika chombo hicho cha Serikali hivyo aondolewe kwa kuwa amekuwa akiiongoza NECTA anavyotaka yeye ikiwa ni pamoja na kuwafukuza ovyo wafanyakazi.

Kwa mujibu wa Missanga, tangu mwaka 2005, Dk Ndalichako amefukuza wafanyakazi 118 NECTA na ameajiri wa kwake 180, na amedai kuwa walioajiriwa wanatoka katika kabila lake ( la Dk Ndalichako).

Alihoji ni kwa nini Dk Ndalichako hajiuzulu kwa kuwa baraza hilo limekuwa na matatizo mengi yakiwamo ya kuvuja kwa mitihani.

Mporogomyi amesema, baraza limeajiri wafanyakazi 79 kutoka mikoa mbalimbali na si wenye asili ya Singida pekee. “Na mimi sidhani kama tunataka mgongano humu ndani” amesema.
Mbunge huyo amesema, analolizungumza ndilo analoliamini na limetoka moyoni mwake.

Leo mchana, Missanga ameomba muongozo wa Spika na kuhoji kama ni sahihi Mbunge kumjibu Mbunge mwenzake aliyechangia jambo bungeni.

Mbunge huyo amesema, mengi aliyoyasema Mporogomyi ni uongo na kusema, baadhi ya wabunge waliowahi kuwa mawaziri wanajisahau na kudhani kuwa bado kwenye madaraka hayo.

Naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda, amemuagiza Missanga afuate utaratibu mwingine kueleza ukweli kuhusu aliyoyasema Mporogomyi.
Makinda amesema, wabunge wanapochangia bungeni wanapaswa kuzungumzia mambo kwa ujumla kwa kutoa hoja badala ya kuwajadili watu.

No comments:

Post a Comment