Monday, March 19, 2012

Slaa aitikisa Arumeru

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alitua Arumeru Mashariki na kuhutubia mkutano uliotikisa eneo la Kwapole – Soko la Ndizi, huku wazazi wa mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari wakipanda jukwaani kujibu matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira dhidi ya mtoto wao.


Mchungaji Samuel Nassari na mkewe, waliwaambia mamia ya watu waliofika kwenye uwanja huo kuwa walitoa baraka kwa Joshua kugombea nafasi hiyo wakisema mtoto wao ni mwadilifu anayefaa kuwawakilisha wananchi wa Arumeru Mashariki bungeni.


Kauli ya Mchungaji Nassari inatokana na matamshi ambayo yamekuwa yakitolewa na Wassira katika kampeni za kumnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari kwamba mgombea wa Chadema hana nidhamu na kwamba amewachosha wazazi wake kwa kutokuwa na nidhamu.


Lakini jana, baba wa mgombea huyo akiwa na mkewe jukwaani alisema:


“Mimi siyo mwanasiasa, lakini nimelazimika kupanda jukwaani leo kutokana na matamshi yaliyotolewa na Wassira, napenda kusema hivi Joshua alipata baraka za familia.”


Alisema kabla ya kugombea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifika nyumbani kwake Songoro na kuwaeleza kuwa wanamtaka Nassari kugombea tena na kusema kwamba familia ilikubali na kumpa baraka zote ikiwa ni pamoja na kuwaita wachungaji kumwombea.


Mchungaji Nassari pia alikanusha madai kwamba mwanaye alikuwa jeuri tangu shule akisema hajawahi kufukuzwa wala kusimamishwa masomo kwa utovu wa nidhamu tangu akiwa shule ya msingi hadi alipohitimu masomo ya shahada, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Mchungaji huyo alisema, mtoto wake alisoma katika shule ya msingi, Sekondari ya Bagamoyo kidato cha kwanza hadi cha nne na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora kidato cha tano na sita.


“Alipokuwa chuo kikuu, ninatambua kwamba alikuwa mtetezi wa wenzake, hivyo ndugu zangu Joshua Nassari anafaa kuwa mbunge na suala kuwa hajaoa halina msingi kwani mke bora mtu anapewa na Mungu na siyo utashi wake au hamu yake, kwani mke siyo kitunguu cha kununua sokoni,” alisema Mchungaji Nassari.


Mapokezi ya Dk SlaaDk Slaa ambaye alihutubia mkutano wa kampeni kwa mara ya kwanza katika uchaguzi huo mdogo, alilakiwa na mamia ya watu na magari ulianzia Uwanja wa Ndege ya Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) hadi eneo la Kwapori, Kata ya Akheri ambako mkutano huo ulifanyika.


Msafara wa kumsindikiza Dk Slaa kuelekea Uwanja wa Kwapori ulianza mara tu baada ya kuwasili KIA majira ya saa tisa alasiri. Msafara huo uliokuwa umesheheni magari na pikipiki, ulifunga kwa muda Barabara ya Arusha-Moshi katika eneo hilo.


Akihutubia mkutano huo, Dk Slaa alisema Chadema kinataka wakazi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, kumchagua Nassari si kwa sababu ana sura nzuri, bali wanataka kumtuma katika Halmashauri ya Meru na bungeni.


“Halmashauri ya Meru ina tatizo kubwa la ubadhirifu wa fedha za umma, fedha za afya, elimu na barabara zinaliwa na hili nina ushahidi nalo kwa sababu nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kwa hiyo Nassari anatakiwa kwenda kufanya kazi ya kudhibiti wizi huo,” alisema Dk Slaa na kuongeza:


“Hata huko bungeni hatumtumi kwenda kufanya kazi ya Chadema wala Mbowe (Freeman) hapana, hatumtumi kwenda kusinzia wala kuzomea, anatakiwa kwenda kufanya kazi ya watu wa Arumeru ambayo kwa miaka 50 ya Uhuru CCM wameshindwa kuifanya.”


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment