Friday, March 16, 2012

Tendwa- Kauli za Mkapa, Vicent Nyerere hatari

Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, John Tendwa

MSAJILI wa Vyama Vya Siasa nchini, John Tendwa ameelezea kukerwa na malumbano ya Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na Mbunge wa Musoma mjini (Chadema), Vincent Nyerere na kuonya kuwa kauli zao ni hatari na zinajenga chuki ndani ya taifa.


Malumbano kati ya wanasiasa hao, yaliibuka baada ya Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM kudai kuwa kwa kipindi chote alichowahi kufanyakazi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hakuwahi kusikia kama kulikuwa na mwanafamilia anayeitwa Vincent Nyerere.

Juzi, malumbano hayo yalichukua sura mpya baada mtoto wa kiume wa Mwalimu Nyerere, Madaraka kuibuka na kuthibitisha kuwa Vincent ni mdogo wao na ni mwanafamilia ya Mwalimu, kwani ni mtoto wa baba yao mdogo, marehemu Josephat Kiboko Nyerere.


Hata hivyo, Madaraka katika majibu yake mafupi kwa Mwananchi aliyoyatuma kwa barua pepe, aliweka wazi kwamba asingependa kujibu maswali mengine zaidi ya kuthibitisha undugu wake na Vincent, akihofu kuingilia kampeni za uchaguzi mdogo wa Arumeru na kushauri maswali mengine yajibiwe na Mkapa mwenyewe au mbunge huyo.


Akizungumza katika mahojiano maalumu jana na Mwananchi ofisini kwake jijini Dares Salaam, Tendwa alisema kauli ya Mkapa dhidi ya Vincent na majibu ya mbunge huyo, ni kinyume cha siasa zilizotarajiwa katika uchaguzi huo mdogo.


Alisisitiza kwamba kauli hizo zinakuja katika kipindi cha kampeni, jambo ambalo linaweza kuibua chuki katika taifa na kusababisha vurugu ndani ya jamii.


Tendwa ambaye ni mlezi wa vyama vya siasa, alisema kutokana na hali hiyo, viongozi hao walipaswa kutumia siasa za kistaarabu wakati wa kampeni hizo na si kuingiza mambo ya familia.


“Hawa wanazungumza haya katika kipindi hiki cha kampeni, lakini wanapaswa kutambua kuwa jamii inawasikiliza, na kwamba kauli zao zinaweza kuzaa chuki itakayosababisha jamii kugombana au kuamini hayo,”alionya Tendwa na kuongeza kwamba athari za malumbano hayo haziishi kwa vyama vyao bali kwa taifa zima.


Aliwataka wanasiasa kutumia lugha za kawaida katika kampeni zao na si kutoa kashfa, zinazoweza kusababisha migogoro.


Tendwa alisema, ukweli wa kifo cha Mwalimu Nyerere, anayeufahamu ni daktari wake katika hospitali ya Mtakatifu Thomas iliyopo Uingereza, ambako mwasisi huyo wa taifa, alilazwa na kupatiwa matibabu mpaka alipofarikiAlisema wakati Mwalimu Nyerere anafariki , Vincent alikuwa mtoto mdogo na kwamba taarifa hizo alipaswa kusema Chifu Wanzagi.


“Kwanza nashangaa sana, wakati Mwalimu Nyerere anafariki, Vincent alikuwa mtoto mdogo sana na kwamba hawezi kujua taarifa za kifo hicho labda awe amesimuliwa na baba yake Chifu Wanzagi ndiye mwenye jukumu la kuzungumzia kifo cha Mwalimu kwa sababu alikuwa kaka yake lakini, huyu ni kijana mdogo sana,” Tendwa alimshukia Vincent.


Tendwa aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwakumbusha wanasiasa kuwa kanuni na sheria ya maadili walizosaini, zinakataza kuchafuana na kwamba tume hiyo inapaswa kuingilia kati kuwakumbusha wanasiasa kuwa, kipindi cha kampeni siyo cha kuchafuana.



“Vyama vya siasa vyote vilisaini kanuni na sheria za maadili wakati wa kampeni, na kwamba mambo yanayojitokeza sasa ni kinyume na kanuni hiyo,kutokana na hali hiyo wanapaswa kuzungumzia mikakati ya vyama vyao kama vitashinda kwenye uchafuzi na si kuchafuana,”alifafanua.



Tendwa alisema kazi ya ofisi yake ni kuhakikisha kuwa, vyama vya siasa vinafuata sheria na taratibu zilizowekwa ili uchaguzi huo uwe huru na haki jambo ambalo linaweza kupunguza malalamiko na mapingamizi.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment