MAMBO vipi mdau, mimi sijambo, weekend imekwisha, tuombeane heri , tuwe na kiasi, malengo, na mtazamo chanya.
Wanasemaje waungwana hapo, wasalimie, naamini wewe na wadau hapo mpo salama na mambo si mabaya, tupo pamoja.
Kabla ya kuendelea na nilichokusudia kukisema leo, namuomba Mungu atuvushe salama katika safari tuliyoianza ya mchakato wa kupata Katiba mpya ya nchi yetu.
Waasisi wa taifa hili walithubutu kuutafuta uhuru, wakaweza kuitunza amani ya nchi yetu, tusonge mbele tukiwa wamoja.
Busara inahitajika sana katika jambo hili, makundi yote yanapaswa kutimiza wajibu wao kwa uaminifu, umakini, na upendo kwa nchi yao ili mchakato huu usiwe chanzo cha kuwagawa Watanzania, au kusababisha mifarakano na machafuko.
Watanzania wanahitaji muda wa kutosha kufikiria namna ya kukabiliana na kero za kila siku za maisha, kukabiliana na ugumu wa maisha, hawahitaji malumbano na vurugu kwa sababu haviwasaidii kupata maisha bora au kumaliza umasikini.
Matatizo waliyonayo wananchi kwa ujumla wao, na katika kaya moja moja yanatosha, wasibebeshwe mizigo mingine, na nadiriki kusema kwamba dhambi kubwa zaidi inayoweza kufanywa na Watanzania ni kuthubutu kuipoteza amani ya nchi hii.
Wapo waliothubutu kuipoteza amani katika familia zao kwa sababu ya tamaa, na ujinga, leo wanajuta, hawana furaha, wanawatesa watoto, wamejiwekea doa la kudumu hadi watakapotoka katika uso wa dunia hii.
Upo mfano hai wa vijana wenzetu waliofunga ndoa mwaka juzi kanisani, wana mtoto, lakini hivi karibuni walifumaniana saa sita mchana kwenye nyumba ya wageni Kinondoni jijini Dar es Salaam, na sasa wapo kwenye mchakato wa kutalikiana.
Ukifuatilia ‘skendo’ hiyo utabaini ukubwa wa tatizo kwenye jamii yetu kwa sababu wanandoa hao wamekutana gesti ndani, na wote walikwenda hapo na wapenzi wao kuivunja amri ya sita hivyo wote walipanga na wakadhamiria kuisaliti ndoa yao.
Kwa kifupi ni kwamba, mume alisafiri kwenda Arusha kikazi, mke alibaki Dar es Salaam na familia, siku walipofumaniana ilikuwa ndiyo mume anarudi kwa basi hivyo alitarajiwa kuondoka huko asubuhi na alitarajiwa kufika Dar es Salaam jioni, lakini alipata lifti ya mwenzake hivyo waliondoka usiku baada ya mkutano, wakafika asubuhi.
Mke alimtarajia mumewe jioni, akatoka ofisini asubuhi kwenda gesti kukutana na mpenzi wake, na kwa bahati mbaya kwao, mume naye baada ya kufika Dar es Salaam alikwenda hapo hapo kwa lengo hilo hilo la kuisaliti ndoa yake.
Mke wa jamaa na ‘shababi’ wake walifika mapema, wakafanya walichokwenda kukifanya, na wakati wanatoka, mume na ‘la aziz’ wake nao walikuwa wanajindaa kuingia katika chumba hicho hicho, na wakati mume yupo mapokezi, akashuhudia mkewe na jamaa wanatoka chumbani.
Siku njema.
No comments:
Post a Comment