Monday, February 20, 2012

Utata wazidi afya ya Mwakyembe

WINGU zito limetanda kuhusu afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe baada ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, kusema kuwa ripoti ya ugonjwa wa Mwakyembe, anayo mwenyewe na kwamba wizara haina ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, kwa waandishi wa habari.


Lakini wakati Dk Mponda akitoa kauli hiyo, baadhi ya watu wa kada tofauti wakiwamo viongozi wa dini na wasomi, wamekosoa ripoti hiyo ya polisi.Mmoja wa watu hao, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa alisema,"hata mimi simwamini Manumba.


"Malumbano hayo yanakuja wakati Dk Mwakyembe ambaye ni pia ni Mbunge wa Kyela, akitarajiwa nchini jana kwenda India kwa matibabu katika Hospitali ya Apollo.


Mahojiano na Waziri Mponda


Gazeti: Mheshimiwa waziri. Nimekupigia kutaka ufafanuzi kuhusu ripoti iliyotolewa na DCI Manumba kuhusu ugonjwa wa Dk Mwakyembe. Ninyi wizara mnaitambuaje?


Waziri: Kiutaratibu ripoti ya daktari ni ya mgonjwa. Sisi hatujaandika ripoti, muulizeni DCI Manumba awape ufafanuzi kama kuna kitu mnataka kuuliza zaidi kwa alichokizungumza na ninyi waandishi.


Gazeti: DCI Manumba alitoa taarifa kwa waandishi lakini aki-refer (rejea) ripoti kutoka wizarani (afya), baada ya kuwasiliana nanyi, kwa nini wewe usiizungumzie?



Waziri: Narudia tena, muulizeni yeye DCI au Dk Mwakyembe mwenyewe, wao wanaweza kuwapa ufafanuzi.


Gazeti: Tayari Dk Mwakyembe mwenyewe amekwishatoa tamko kwamba ripoti iliyosomwa na polisi, haina uhusiano na ripoti aliyokuwa nayo yeye kuhusu uchunguzi wa maradhi yake. Je, ripoti hii ya polisi ambayo wamedai wameipata kwenu (wizara) mmeitoa wapi?


Waziri: Ni hivi, baada ya daktari kumchunguza mgonjwa, hutoa ripoti na kumpa mgonjwa. Kwa hiyo, ripoti ya Hospitali ya Apollo anayo Dk Mwakyembe mwenyewe. Tena yeye kaeleza vizuri kabisa kwamba hata uchunguzi bado unaendelea. sasa hapo mnataka niseme nini tena?


Gazeti: Sasa kama ripoti anayo Dk Mwakyembe mwenyewe na tayari amesema ripoti ya polisi waliyosema imetoka kwenu siyo sahihi, je wizara iliwahi kupata ripoti ya Hospitali ya Apollo.

Waziri: Sisi tulichokifanya ni kumpa rufaa Dk Mwakyembe kwenda India. Ripoti hadi sasa anayo mwenyewe ingawa huwa tunapata taarifa baada ya yeye mgonjwa kuzileta kwetu. Hizo ndizo kanuni za taaluma ya udaktari, kwa hiyo ripoti anayo mwenyewe.


Gazeti: Sasa kama ripoti anayo Dk Mwakyembe mwenyewe, hii iliyosomwa na DCI imetoka wapi?


Waziri: Kumbuka DCI ana njia zake nyingi za kupata taarifa. Kwa hiyo ndiyo maana nasisitiza, muulizeni mwenyewe awape ufafanuzi kwa aliyozungumza na waandishi. Sisi wizara mnatuonea tu.


Gazeti: Lakini, hata kama ugonjwa ni siri, huoni mheshimiwa waziri kwamba kuna haja ya kuondoa utata kuhusu suala hili ikizingatiwa kuwa Dk Mwakyembe ni kiongozi anayegusa hisia za watu tofauti?


Waziri: Wanaoweza kuzungumzia maradhi yake, ni familia yake au yeye mwenyewe kwani ndiye mwenye ripoti. Mtafuteni au iulizeni familia yake iwapatie majibu. Lakini wizara haiwezi kufanya hivyo. Narudia tena, kuhusu hilo la DCI muulizeni mwenyewe awape ufafanuzi, mimi sijaona ripoti ya DCI aliyozungumza na waandishi wa habari.


Akizungumza na waandishi mwishoni wa wiki iliyopita, Manumba alisema, “ukweli kuhusu kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu, tumeupata baada ya kuwasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo nayo imewasiliana na hospitali aliyokuwa amelazwa Dk Mwakyembe nchini India.


Taarifa zinaonyesha kuwa hakuna sumu." Jana, alipoelezwa kwamba Dk Mwakyembe ameikana ripoti yao, Manumba alisema "sasa suala hilo litashughukiliwa kisheria."


Alisisitiza kuwa suala hilo litashughulikiwa kwa kufuata misingi ya kisheria na kwamba, Jeshi la Polisi haliko tayari kuendeleza malumbano kupitia vyombo vya habari.


"Hatua zaidi zinachukuliwa dhidi ya jambo hilo, kwa sasa litashughukiliwa kwa kufuata misingi ya kisheria kama nilivyokwishaeleza awali,"alisema Manumba.


Kauli ya Dk MwakyembeJuzi, akitoa tamko baada ya kukerwa na kauli ya Jeshi la Polisi alisema mbunge huyo alisema ‘napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”!


"Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari, hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya Apollo inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti au kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”Dk Mwakyembe pia alitoa sababu kuu tatu za kupinga ripoti o ya DCI akisema:


"Kwanza, kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake, unaoendelea katika Hospitali ya Apollo, nchini India, ambako bado sijahitimisha matibabu yangu, pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu.


Alisema sababu ya tatu ni kitendo cha Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima sasa, halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment