Monday, February 20, 2012

Slaa- Mwakyembe kafanyiwa kama mimi

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa amesema , hana imani na ripoti ya uchunguzi iliyofanywa na Jeshi la Polisi na kutolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, kuhusu hali ya Mwakyembe.


"Mimi siwezi kuzungumzia ugonjwa wa mtu, lakini niseme tu kwa kifupi kuwa ripoti ya DCI Manumba siwezi kuiamini. Sina imani na Manumba kwa sababu mimi mwenyewe imenitokea,"alirusha kombora kwa Manumba.


"Niliwekewa vipaza sauti kwenye kitanda changu mjini Dodoma, taarifa za tukio hilo zilifika kwake lakini hadi leo hajatoa majibu yoyote ya uchunguzi wake," alisisitiza.


"Nani asiyemfahamu Manumba ndiye alishuhudia watu 50 wakipoteza maisha kwa kufukiwa mgodini na kesi ikaenda mahakamani, ikafutwa, Kwa nini Serikali yetu inamweka mtu wa aina hiyo kwenye nafasi kubwa kama hiyo," alihoji Dk Slaa.


Alisema hata katika tukio la kuwekewa vinasa sauti kwenye kitanda huko Dodoma, hakuwahi kuitwa na kuhojiwa.Askofu Ruwa'ichAkizungumzia mvutano huo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Yuda Thadeus Ruwa'ichi, alisema kinachoendelea kati ya jeshi na Dk Mwakyembe, ni ishara ya kutosha kuwa taifa liko kwenye ubabaishaji."Malumbano hayo yanaonyesha kuwa taifa liko kwenye ubabaishaji na hiki siyo kitu kizuri.


Ushauri wangu turudi na kuwa wakweli, tufanye kazi kwa uadilifu,"alisema askofu Ruwa'ichi. Rais huyo wa TEC, pia aliwataka waandishi wa habari kufanya uchunguzi wao na kutoa taarifa za kubaini ukweli kuhusu jambo hilo, ili kuondoa utata uliopo.Jukwaa la katibaMwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alielezea kushangazwa kwake juu ya nguvu aliyopata Manumba ya kupishana na mawaziri.


Alisema kinachotakiwa ni jopo la madaktari bingwa wa nchini, kuunda tume ili kuja na jibu litakalowawezesha wananchi waache kuihofia Serikali."Mabishano baina ya viongozi wa Kikwete (Rais), yanaonyesha dhahiri kwamba Serikali ina ulegevu, unaotokana na kiongozi wake mkuu kukaa kimya," alisema.


Kibamba alisema wakati umefika kwa Rais wa nchi kujitokeza hadharani na kuwawajibisha mawaziri, kama anaamini kuwa yanayoongelewa ni ya uwongo.


“Kilichoelezwa na Manumba hakiingii akilini kwa mwananchi wa kawaida, hii nchi sasa ni ya kisanii maana umegeuka mchezo wa Bongo land wa kuongea bila kuthitibishwa na madaktari bingwa,”alisema.


“Afya za mawaziri si suala la siri hasa ikizingatiwa kuwa wanatumia fedha za Watanzania katika kutibiwa . Kama kiongozi anataka kuweka siri aondoke kwenye uongozi atumie fedha zake,” alisisitiza.


“Siamini kama DCI Manumba ni daktari , kinachotakiwa ni kuundwa jopo la madaktari bingwa na Rais kuwaeleza Watanzania kinachowasibu viongozi wake,” aliongeza.


Alisema Watanzania wanaamini kuwa Dk Mwakyembe alilishwa sumu na kwamba ni vema Serikali ikaondoa mkanganyiko huo.Akizumngumzia sakata hilo kwa njia ya simu, Mbunge wa Nyamagana, jijini Mwanza, Hezekiah Wenje alisema ni dhahiri kwamba kuna kitu ambacho Jeshi la Polisi linakificha.


“Hali halisi inaonyesha wazi kuwa kuna ukweli mwingi unaofichwa na Jeshi la Polisi na ndiyo maana kunakuwa na upotoshaji wa wazi,” alisema Wenje.Mbunge huyo alisema kuna haja sasa ripoti ya madaktari kuwekwa wazi ili watu wajue.


Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea mkoani Mwanza, Stephen Magoiga alisema Jeshi la Polisi, linaonyesha wazi kwamba lina matatizo makubwa ya kiutendaji linapotaka mlalamikaji kuwasilisha ushahidi.


Akikumbushia Dk Mwakyembe kudaiwa ushahidi alipopeleka malalamiko yake juu ya maisha yake kuwa hatarini, Magoiga alisema ushahidi ni suala la kitaalamu ambalo si mtu yoyote anaweza kukusanya.


“Jeshi la Polisi ndilo lenye utaalamu wa kukusanya ushahidi na wanalipwa kwa kazi hiyo, sasa wanapodai mlalamikaji alete ushahidi na baadaye kupingana na madai yake, ni dhahiri kwamba jeshi hilo linasema uwongo,” alisema Magoiga.


Alisema polisi wanapaswa kufanya kazi kisayansi kwa kuzingatia kwamba tuhuma za Dk Mwakyembe kulishwa sumu zimetolewa mara ya kwanza na mtu mzima mwenye hadhi yake katika jamii ya Kitanzania.


Alisema ni jambo la kushangaza kuona polisi wakioonyesha dharau za waziwazi kwa tuhuma zilizotolewa na mtu kama Waziri Samwel Sitta.“Kama kauli ya Sitta inaweza kutendewa hivi na polisi je, ya mtu wa kawaida itakuwaje," aliohoji wakili huyo.


Ijumaa iliyopita Manumba alitoa tamko kuhusu kauli zilizowahi kutolewa na Sitta akiziita kuwa ni za uwongo na kuwataka watu wazipuuze.


Pia alitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Waziri huyo wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala, alisema mabishano yanayoendelea ndani ya Serikali, yanaonyesha kuwa kuna kitu kinachofichwa.


Profesa Mpangala alihoji kuhusu mahali ambako kumpa nguvu Manumba kuongelea afya ya Dk Mwakyembe.Alisema kitendo hicho kinapingana na msimamo wa


Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye aliwahi kukaririwa akisema Dk Mwakyembe ndiye anayepaswa kueleza hadharani maradhi yanayomsumbua.


Alisema Jeshi la Polisi limedharau kauli ya Pinda na kwamba hiyo inaonyesha kuwa Serikali, imekosa msemaji wa mwisho.


Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaamShehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Musa Salim, alisema hatua ya viongozi kupishana inaonyesha kuwa hawafanyi kazi kwa umoja.


“Kilichoongelewa na Jeshi la Polisi ni sahihi kwa sababu limepewa jukumu la kuchunguza na kama kuna viongozi hao wanapinga majibu hayo, nadhani wanapaswa kuja na jibu,” alisema.


“Mimi sijui chochote lakini kama unachoeleza ni hivyo, maoni yangu ni kwamna tunatakiwa kuheshimu uchunguzi wa polisi ambao wamepewa dhamana ya kuchunguza,” alisema Sheikh Salim.


Historia ya ugonjwawa MwakyembeDk Mwakymbe alianza kuumwa Oktoba 9 mwaka jana na baadaye kupelekwa India ambako alilazwa katika Hospitali ya Apollo kwa matatibu.


Alirejea nchini Desemba 11 mwaka jana, baada ya kulazwa hospitalini kwa takribani miezi miwili.



Msemaji wa familia ya Dk Mwekyembe ambaye ni Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa alisema mara baada ya mbunge huyo wa Kyela kuwasili nchini kuwa, afya yake ni nzuri na ndio maana ameruhusiwa kutoka hospitalini.



Kauli za Waziri SittaMara kadhaa Waziri Sitta amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza kuwa ugonjwa wa Dk Mwakyembe, umetokana na kulishwa sumu.


Akiwa kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa kiongozi, iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, Jijini Dar es Salaam Januari 28 mwaka huu, Sitta alisema “ Dk Mwakyembe kapewa sumu, kama vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze ukweli, tena haraka.”


“Ni vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini, mhudumu anakuja kuufagia, lakini baada ya saa moja unarudia tena, kitu hicho si cha kawaida,” alisisitiza Sitta.


Sitta alisema wamejaribu wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote.



Waziri NahodhaHata hivyo, akijibu moja ya kauli hizo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nohodha alimtaka Waziri Sitta awasilishe ushahidi wake ili ufanyiwe kazi badala ya kuzungumza nje ya vyombo vya sheria.


Lakini, Sitta alisema hatapeleka ushahidi kuhusu madai kwamba Dk Mwakyembe alilishwa sumu kwa kuwa polisi tayari wana ushahidi.Alilaumu kuwa hata yeye aliwahi kupeleka tuhuma za kutaka kuawa lakini alipuuzwa.




Alisema inachotakiwa kufanywa na polisi ni uchunguzi kuhusu madai ya Dk Mwakyembe kulishwa sumu.



“Waziri Nahodha anataka ushahidi gani ikiwa taarifa za madaktari zinazomhusu Dk Mwakyembe kuhusu sumu aliyopewa zilishapelekwa polisi, anataka mimi nitoe ushahidi gani,” alisema Waziri Sitta.


Chanzo: Gazeti la Mwananchi

No comments:

Post a Comment