Tuesday, June 14, 2011

Bunge moto

MBUNGE wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila, jana jioni alichafua hali ya hewa bungeni mjini Dodoma baada ya kuwataja wabunge wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa aliwakamata wanaomba katika halmashauri.


Kafulila alikuwa anachangia hoja ya Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano, akawataja Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Mbunge wa Bahi, Omary Badwel wote wa CCM akidai kuwa aliwakamata wakiomba rushwa kwa viongozi wa Halmashauri ambayo hakuitaja.


Wakati anataja majina hayo, Mwenyekiti wa Bunge, George Simbachawene, alimuamuru Kafulila akae kwa kuwa muda wake wa kuchangia ulikuwa umekwisha.


Mbunge huyo hakutii amri ya Mwenyekiti wa Bunge, akaendelea kuzungumza bila kujali kengele ya pili iliyopigwa kuashiria kwamba muda wake wa kuzungumza ulikuwa umekwisha.


"Mheshimiwa Mwenyekiti kwa wakati wa sasa ni vigumu kusimamia matumizi kwani mfumo wetu wa uongozi unaruhusu ufisadi, wapo viongozi, mawaziri, wabunge wanaomba rushwa...."

alisema Kafulila.


Kauli hiyo iliamsha zogo bungeni lililoambatana na sauti zisizo rasmi katika ukumbi wa Bunge zikiuliza ".....wapo humu humu?" Kafulila alijibu "Ndiyo..."


Sauti moja ilisema wataje, hapo ndipo aliposema "....Wapo kina Zambi, Badwel, nimewakamata na nimechukua hatua, hatuwezi kuendelea namna hii," kisha akakaa.


Baada ya dakika chache tangu alipoketi, Kafulila alionekana akiteta jambo na Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali na Augustine Mrema wa Vunjo na baadaye Mkosamali aliomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, akitaka waliotuhumiwa watajwe ili wafahamike vizuri.


Zambi na Badwel ni wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa pamoja na Kafulila chini ya Mwenyekiti wao, Mrema.


"... Mwenyekiti, tumesikia tuhuma zilizotolewa hapa kuhusu rushwa, naomba mwongozo wako maana hapa tumesikia juu juu tu...,"alisema Mkosamali.


Mwenyekiti wa Bunge, Simbachawene akijibu hoja hiyo alisema atatoa mwongozo wake baadaye, katika muda ambao ataona unafaa.


Kauli ya Naibu Spika, Job Ndugai alisema taarifa ya tuhuma za rushwa kwa wabunge ziliwahi kutolewa katika kikao cha Kamati ya Uongozi na Mrema, ijapokuwa majina ya watuhumiwa na mlalamikaji hayakutajwa.


"Kama Mheshimiwa Spika aliandikiwa barua mimi sifahamu, lakini nakumbuka katika moja ya vikao vya kamati ya uongozi suala hili liliwahi kuelezwa na nadhani tukio hili linadaiwa kwamba lilitokea huko mkoani Tanga, kama sikosei na ilikuwa ni kama taarifa tu,"alisema Ndugai na kuongeza:


"Lakini Mrema alisema mlalamikaji alikuwa na ushahidi na akasema alikuwa na mpango wa kuwasiliana na Takukuru (Taasisi na Kuzuia na Kupambana na Rushwa) na sisi kwa kuona limekaa hivyo hatukuwa na mjadala tukadhani huko ndiko mahala pake."


Ndugai alisema msingi wa suala hilo kuwasilishwa kama taarifa katika kikao hicho, ulikuwa kutoa tahadhari kwa Kamati za Bunge zinazoshughulikia Hesabu za Serikali, kujihadhari ili zisitumbukie katika kashfa za rushwa na kuharibu sifa nzima ya Bunge.


Awali, Kafulila alisema tayari taarifa za tuhuma hizo za rushwa zilikuwa zimefikishwa kwa Spika kwa maandishi pamoja na Mrema kwa ajili ya hatua zaidi.


Kadhalika, Mbunge huyo alisema taarifa hizo zilikuwa zimekwishawafikia viongozi wa juu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na kwamba aliwahi kukutana na Spika kuhusu suala hilo ijapokuwa hakukuwa na hatua zozote ambazo zilichukuliwa.


Zambia amesema, taarifa hizo zimemsikitisha na kwamba anasubiri hatua za kibunge kwa kuzingatia kanuni ya 63.


"Nimemsikia akizungumza, taarifa hizo zimenisikitisha sana kwani kama alivyosema kwamba alitukamata, alikuwa anasubiri nini kutotoa taarifa wakati wote, au alikuwa akisubiri kutuumbua? Mimi nasubiri hatua za kibunge na nadhani kabla ya kufikia mwisho wa kikao cha leo, Mwenyekiti atatoa mwongozo,"amesema Zambi.


Badwel amesema, hakumbuki kuwapo kwa tukio la namna hiyo na kwamba wakiwa mkoani Tanga walizichukulia hatua halmashauri zote nne ambazo walizikagua na kukuta udhaifu katika usimamizi wa fedha.


"Kwani yeye alitukamata ni Polisi au Takukuru? Kwanza Tanga hivi vyote havipo? Sisi tumefanya kazi nzuri sana kama mnavyojua Kamati ya LAAC imefanya kazi nzuri tu, sasa huyo anatafuta umaarufu tu na kauli zake zinalenga kutuchafua,"amesema Badwel kwa simu.

No comments:

Post a Comment