MTANGAZAJI wa Redio Times FM, inayomilikiwa na Kampuni ya Bussiness Times Ltd, Hadija Shaibu, maarufu kwa jina la ‘Dida wa Mchops’ anashikiliwa na askari wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya cha Jeshi la Polisi baada ya kumshuku kuwa anasafirisha dawa za kulevya.
Kuna madai kuwa Dida alikamatwa Juzi Jumatatu baada ya askari wa kitengo hicho waliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kumkamata wakati akijiandaa kupanda ndege kwenda China.
Habari zilieleza kuwa Dida alikuwa akijiandaa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopian Airline, lakini polisi walilazimika kumtia nguvuni baada ya kumpeleleza kwa muda mrefu na kuhisi kuwa huenda siku hiyo alikuwa amemeza dawa hizo ili azisafirishe nje ya nchi.
Inadaiwa kuwa, baada ya Dida kukamatwa, alipelekwa kwenye choo maalumu kilichopo uwanjani hapo ambacho hutumiwa na askari wa kitengo hicho kuwahifadhi watuhumiwa wanaowakamata wakiwa wamemeza dawa za kulevya kwa muda ambapo endapo mtuhumiwa alikuwa amemeza dawa hizo atazitoa wakati akijisaidia.
Taarifa zaidi zilieleza kuwa tangu alipoingizwa kwenye choo hicho juzi jioni hadi jana saa nne asubuhi, hakuweza kugundulika kuwa na dawa hizo tumboni ambapo alichukuliwa hadi makao Makuu ya Kitengo hicho, huko Barabara ya Kilwa kwa ajili ya kuhojiwa.
Taarifa zilizopo zinadai kuwa hajakutwa na pipi hata moja, na alidhaminiwa jana jioni.
No comments:
Post a Comment