Sunday, November 25, 2012

Zitto atoa mazito ya moyoni mwake



MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amesema, ili Tanzania iwe salama, ni lazima CCM ishindwe katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.

Zitto aliyasema hayo katika mahojiano ya moja kwa moja baina yake na mtandao wa kijamii wa Jamii Forum (JF).

“Ili Tanzania iwe salama, ni lazima CCM ishindwe uchaguzi. CCM ikishinda tena mwaka 2015 itavunja sana moyo wa wananchi na wengine wanaweza kukata tamaa. 

“Lakini pia CCM imechoka na haina nguvu za kutosha kukabiliana na changamoto za nchi hivi sasa. Njia pekee ya kuisaidia CCM iweze kujipanga upya ni yenyewe kuondoka madarakani. 



 

“CHADEMA ina nafasi kubwa sana ya kushinda na kuongoza dola. Muhimu chama kijipange na kuonekana kama chama kilichotayari kushika dola. Tuyatende tunayoyasema na tujiimarishe zaidi.

Zitto amesema, licha ya Tanzania kuwa na vyama vya siasa visivyopungua 20 hivi sasa, mbele ya safari haoni uhai wa vyama zaidi ya vinne. Amevitaja vyama vikubwa vitakavyosalia kuwa ni CCM na CHADEMA

“Huko mbele ninaona Tanzania yenye vyama sio zaidi ya vinne. Vyama vikubwa viwili, CCM na CHADEMA. CUF watakuwa ‘balancing party’ kama ilivyo LibDems UK au Greens na Liberals Ujerumani.  
 
Zitto amekanusha kuwa na uhusiano na CCM, na kusema kuwa hiyo ni propaganda inayofanywa na watu wachache wenye nia ovu dhidi yake.

“Ukitaka kummaliza mwanasiasa yeyote wa upinzani hapa Tanzania, mhusishe na ama usalama wa Taifa au CCM. 

“Ndivyo ilivyokuwa kwa Mabere Marando miaka ya tisini. Marando ameishia kuweka sawa historia ingawa propaganda dhidi yake zilikuwa kali sana kiasi cha kuogopwa kweli kweli. Napita njia hiyo hiyo ya Marando na wanaonipaka matope haya wataona aibu sana ukweli utakapodhihiri.

“Siku za mwisho za uhai wake ndugu Chacha Wangwe naye aliambiwa ni CCM na kwa kweli alikufa akiwa na chuki sana kuhusu tuhuma hii.

“Faida kubwa niliyonayo mimi ni kwamba, mtaji wangu wa kisiasa ulikuwa ni mkubwa mno na ndiyo maana tuhuma hizi hazijaniathiri. 

“Ninaamini tuhuma kama hizi zingekuwa kwa watu wengine, wangekuwa wameshafutika kwenye historia ya siasa. 

“Sijawahi kuwa mwana CCM, familia yangu yote kabisa ni waanzilishi wa CHADEMA. Sina historia na CCM. Inawezekana wanaosema mimi ni CCM wengi wao wamewahi kuwa CCM, wana familia zao ndani ya CCM na wamewahi kula matunda ya CCM. Mimi sijawahi na wala sitawahi.

“Baadhi ya watu wanapandikiza chuki hizi kwa sababu zao wenyewe. Hawanisumbui maana najua ni kikundi kidogo cha watu wachache wenye malengo yao ovu. Wajue tu kwamba hawawezi kuwadanganya Watanzania ambao wanafanya maamuzi yao yasiyotokana na propaganda ila kutokana na matendo ya kila mmoja. 

“Onyo: Watu hao hawawezi kummaliza Zitto kisiasa bila kuiathiri CHADEMA, maana the image of Zitto is so intimately intertwined with CHADEMA that you couldn’t attack Zitto without jeopardizing the image of Chadema, and vice versa,” alisema.

No comments:

Post a Comment