Tuesday, May 22, 2012

Waziri akuta madudu Maliasili, aomba msaada

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki (kushoto) akiwa na Naibu Wake, Lazaro Nyalandu siku walipoanza kazi rasmi katika Wizara hiyo.

WAZIRI mpya wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, ameshtushwa na ubadhirifu wa kutisha katika wizara hiyo, hususani Idara ya Wanyamapori unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji wake.

Waziri Kagasheki amewaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa, idara hiyo inanuka kwa uozo unaotokana na wizi na ubadhirifu mkubwa ambao umeleta hasara kwa taifa.
Aliyasema hayo baada ya kuzindua Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) jijini Dar es Salaam, jana

Kagasheki alidai Idara ya Wanyamapori  inaongoza kwa madudu ya kutisha katika wizara hiyo na kwamba, fedha zilizotafunwa na wajanja hao ni nyingi.

“Jamani Idara ya Wanyamapori ina fedha nyingi, lakini zinaliwa na watu kwa maslahi binafsi, na kama fedha hizo zingekuwa zinapelekwa serikalini kama inavyohitajika, nchi hii kwa sasa ingefika mbali, mimi naogopa hata kutaja kiasi cha fedha hapa hadharani,” alisema.

  Balozi Kagasheki amesema , usafirishaji wanyamapori nje ni mkubwa mno licha ya serikali kusitisha biashara hiyo.

Alisema , biashara ya kusafirisha wanyama pori inafanywa kati ya wafanyabiashara wa ndani na baadhi ya watendaji, ambao hawajali na wanaonekana kutumia kila mbinu kuifanikisha.

Balozi Kagasheki alionesha hofu yake ya kukabiliana na wafanyabiashara na baadhi ya maafisa wa wizara hiyo,na ameomba msaada kutoka taasisi nyingine, vikiwemo vyombo vya habari kusaidia kupambana na ‘genge’ la wabadhirifu hao.

“Katika idara kunahitaji usaidizi maana hapa ni vita, na hata ninyi waandishi nafikiri mnaweza tukasaidiana kwa kuwa najua mtakuwa mnawajua sana wafujaji. Kuwaondoa hawa ni kutangaza vita,” alisema.

Amesema, atavunja uongozi wa idara hiyo na kuiunda upya haraka.

Alisema ataagiza kufanyika kwa sensa kwa wanyama na kuweka wazi kila kitu, ili kunusuru kumalizika kwa wanyama wote.

“Tutawajulisha wananchi waelewe, hatutachelewa maana watu wameshajua, wasije kuwamalizia wanyama wote,” alisema Balozi Kagasheki.

No comments:

Post a Comment