Wednesday, April 18, 2012

Milioni 70/- zatumika kumzika Steven Kanumba

Steven Kanumba

Jeneza lenye mwili wa Kanumba


Mama mzazi wa Steven Kanumba akiuaga mwili wa mwanae


KAMATI ya mazishi ya aliyekuwa msanii maarufu nchini, Steven Kanumba, imesema imetumia Sh milioni 70/- kugharimia mazishi na maziko ya msanii huyo nyota wa filamu Tanzania.


Kanumba aliaga dunia usiku wa kuamkia Aprili 7 nyumbani kwake Sinza, Dar es Salaam, akazikwa Aprili 10 katika makaburi ya Kinondoni, jijini humo.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mtitu Gabriel amesema, kamati hiyo iliyoratibu mazishi ya msanii huyo tangu Aprili 7, ilikusanya michango na ahadi za takribani Sh milioni 90 huku gharama za mazishi hadi maziko vikigharimu Sh 70,502,000.


Mtitu amesema, Kamati hiyo ilitumia Sh 52,102,000 na ahadi za malipo ya vifaa ambazo ni Sh 18,400,000 na zilitumika kwa vifaa mbalimbali zikiwamo taa, jukwaa, viti na maturubai.


Kwa mujibu wa Mtitu, Sh milioni nne zilizobaki miongoni mwa fedha zilizokusanywa zilikabidhiwa kwa mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa na kwamba, ahadi ya Sh milioni 15.5 bado haijatimizwa.


Amesema, ingawa Kanumba alikuwa maarufu, alikuwa masikini na si tajiri kama ilivyokuwa inafikiriwa.


“Pamoja na jina la Kanumba kuwa kubwa, hakuwa na fedha, na ndiyo maana baada ya kutoka kuhifadhi mwili wake Muhimbili, tulijikusanya na kujipanga kuhakikisha tunampumzisha kwenye nyumba ya milele kwa heshima ya hali ya juu na hili tumelifanikisha,” alisema Mwenyekiti huyo.


Amesema, Kamati hiyo ilianza bila hata Sh 100 na hivyo wanakamati walibeba gharama za awali.


“Tulitambua mchango mkubwa wa Kanumba enzi za uhai wake, tuliona iko haja ya kufanya yote haya, tulianza tukiwa hatuna hata Sh 100, ingawa baadaye Kamati ilichangia gharama za awali ambazo zilipatikana miongoni mwa wajumbe wenyewe,” alieleza.


Amesema, kamati ilikadiria kuwa watu wapatao 40,000 wangehudhuria mazishi na maziko ya Kanumba kutokana na idadi ya watu ambao walikuwa wakifika msibani Sinza, lakini wingi wa watu na ufinyu wa muda siku hiyo ndivyo vilifanya utaratibu kuaga mwili ukatizwe.


“Wakati wa mazishi tulikuwa tunahudumia waombolezaji 3,000 mpaka 4,000 kwa siku, hivyo tukaweka makadirio ya watu 40,000 siku ya maziko, lakini watu waliojitokeza walikuwa wengi na ikawa vigumu kutoa nafasi kwa wote kuaga, hasa kutokana na wingi na mazingira yalivyokuwa na muda pia,” alifafanua.


Kamati iliyoratibu shughuli zote za mazishi iliundwa na wadau wa filamu, wasanii, wafanyabiashara, ndugu na marafiki wa Kanumba, aliyekuwa mwigizaji nyota wa filamu nchini na aliyevuma pia katika nchi mbalimbali barani Afrika.

No comments:

Post a Comment